Wednesday, September 26, 2012

5:14 PM
Coastal Union

Na Prince Akbar
COASTAL Union imeibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Kagera Sugar ya Bukoba, kwenye  Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga, katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Ushindi huo, ulitokana na mabao ya Daniel Lyanga na Nsa Job mawili, ni wa pili katika mechi nne za Wagosi wa Kaya tangu kuanza kwa Ligi Kuu, unakuja siku moja baada ya kujiuzulu kwa aliyekuwa Kocha Mkuu wa timu hiyo, Juma Mgunda.
Mgunda, alijiuzulu jana akisema ameamua kufanya hivyo mapema, kabla ya mambo hayajaribika, ili mwalimu mpya anayekuja afanye kazi vizuri.
Akizungumza na BIN ZUBEIRY jana, Mgunda alisema kwamba anaachia timu baada ya kucheza mechi tatu za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, akiwa ameshinda moja na kutoa sare mbili.
“Kama utaweza kuona naiacha timu ikiwa kwenye hali nzuri kuliko Yanga, ambao wamefungwa mechi moja, sare moja na kushinda moja, naondoka kwa moyo mkunjufu, sina kinyongo na mtu,”alisema.
Mgunda alisema hiyo ndio hulka yake tangu anacheza Coastal Union, kuwa na moyo swafi na ataendelea kuwa hivyo. “Mimi ni mpenzi wa Coastal Union, hakuna asiyejua, na kwa manufaa ya timu, naondoka,”alisema.
Kumekuwa kama kuna kampeni ya kumvuruga Mgunda kazini ambayo imekuwa ikiendeshwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga kwa kumzomea kila timu inapocheza, hatimaye ameamua kuwaachia timu.
Kwa sasa Coastal, imebaki na kocha Msaidizi, Habib Kondo ambaye msimu uliopita alikuwa kocha wa Villa Squad ya Kinondoni, iliyoshuka daraja na leo ndio kaiongoza timu  hiyo ya Barabara ya 13, katika mechi na Kagera Sugar.
Mgunda anakuwa kocha wa pili wa Ligi Kuu kuachia timu, baada ya Mbelgiiji, Tom Sainftiet ambaye amefukuzwa Yanga, baada ya kutofautiana na uongozi, akiwa ameiongoza timu kwenye mechi mbili tu za Ligi Kuu, akitoa sare moja na kufungwa moja. Hemed Morocco, kocha wa Mafunzo ya Zanzibar yupo kwenye mazungumzo na uongozi wa Coastal Union ya Tanga, ili awe kocha mpya wa timu hiyo kufuatia kubwagwa manyanga kwa Mgunda.
Katika mechi nyingine ya ligi hiyo, Polisi Morogoro imelazimishwa sare na Toto African ya Mwanza kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro jioni hii.

0 comment.:

Post a Comment