BAO pekee la Nahodha Nadir Haroub Ali ‘Cannavaro’ jioni hii limeipa ushindi wa 1-0 Yanga SC katika mchezo wa kwanza wa kuwania kucheza Hatua ya 16 Bora Ligi ya Mabingwa Afrika, dhidi ya Al Ahly ya Misri Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Cannavaro alifunga bao hilo dakika ya 87 akimalizia kona maridadi ya winga Simon Msuva kutoka wingi ya kulia.
Kona hiyo ilitokana na kipa Sherif Ekram Ahmed kupangua shuti kali la mshambuliaji Mganda, Emmanuel Okwi.
Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Heileyesus Bazeze aliyesaidiwa na Kindie Mussie Tdedesse Shawangiza wote kutoka Ethiopia, hadi mapumziko milango ilikuwa migumu.
Shujaa; Beki Nadir Haroub 'Cannavaro' akipongezwa na wenzake Emmanuel Okwi na SImon Msuva baada ya kufunga bao pekee jioni dhidi ya Al Ahly |
Yanga SC ndiyo waliotawala zaidi mchezo na kutengeneza nafasi kadhaa nzuri za kufunga, lakini wakakosa umakini katika kumalizia.
Simon Msuva alikuwa chanzo kizuri cha mashambulizi ya Yanga upande wa kulia, lakini Waganda Emannuel Okwi na Hamisi Kiiza walishindwa kutumia nafasi.
Haruna Niyonzima, Frank Domayo na Mrisho Ngassa kwa pamoja walicheza vizuri katika safu ya kiungo kipindi cha kwanza.
Kipindi cha pili, Ahly kidogo walibadilika na kuongeza kasi ya mashambulizi kupitia kwa Amr Gamal, ambaye hata hivyo alidhibitiwa vikali na walinzi wa Yanga, ambao leo walicheza kwa umakini wa hali ya juu.
Mabadiliko yaliyofanywa na kocha Mholanzi Hans van der Pluijm, kumuingiza mshambuliaji Didier Kavumbangu kuchukua nafasi ya Hamisi Kiiza yalifufua makali ya safu ya ushambuliaji ya timu hiyo.
Winga wa Yanga SC, Simon Msuva kushoto akimtoka beki wa Al Ahly |
Mshambuliaji wa Yanga SC, Emmanuel Okwi akiwatoka mabeki wa Ahly |
Kavumbangu aliwapa wakati mgumu mno mabeki wa Ahly tangu alipoingia dakika ya 66 hata mashabiki wa Yanga wakatamani angekuwa uwanjani tangu mwanzo.
Pamoja na kufungwa 1-0, Al Ahly inayofundishwa na kocha Mohamed Yousef, ilionyesha upinzani kwa Yanga SC, jambo ambalo linaashiria katika mchezo wa marudiano lolote linaweza kutokea.
Baada ya matokeo haya, Yanga SC sasa inahitaji sare ya ugenini ili kusonga mbele hatua ya 16 Bora.
Kihistoria hii inakuwa mara ya kwanza kabisa Yanga SC inapata ushindi dhidi ya timu ya Misri na Kaskazini mwa Afrika kwa ujumla, kwani mara zote imekuwa ikifungwa na kutoa sare.
Kikosi cha Yanga SC leo kilikuwa; Deo Munishi ‘Dida’, Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Frank Domayo, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Hamisi Kiiza/Didier Kavumbangu dk66, Emmanuel Okwi na Mrisho Ngassa/Said Bahanuzi dk87.
Al Ahly; Sherif Ekramy Ahmed, Saad El-Din Saad, Mohamed Ghareeb, Ahmed El Moneim, Sayed Abdel Waheed, Shihab Eldin Saad, Hossam Mohammed, Ramy Abdel Aziz, Moussa Yedan/Mahmoud Ibrahim dk59, Mohamed Ismail/Ahmed Shakri Abdelraouf dk 73 na Amri Gamal Sayed/Ahmed Raoud Adam dk88.
0 comment.:
Post a Comment