Wednesday, September 19, 2012

3:48 PM

Yanga sport club na Simba sport club kazi kwenu sasa


KAMPUNI ya Bia Tanzania kupitia Bia ya Kilimanjaro Premium Lager hatimaye inatarajia kukabidhi mabasi mapya ya kisasa  kwa timu za Simba na Yanga siku ya Ijumaa asubuhi.

Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, George Kavishe alisema jana kuwa maandalizi yote yamekamilika na makabidhiano hayo yatafanyika katika viwanja vya ofisi za TBL Ilala.

“Zaidi ya wageni 100 wamealikwa kwenye hafla hii itakayofanyika Ijumaa hapa TBL na kati ya hawa wageni kutakuwa na baadhi ya mashabiki wa timu hizi mbili kwa hivyo tunatarajia makabidhiano ya aina yake,” alisema Kavishe.

Kwa mujibu wa ratiba, baada ya makabidhiano, kila timu itaondoka na basi lake na wachezaji na mashabiki na kupita katika matawi yao kwa msafara maalumu utakaoambatana na burudani mbalimbali huku mashabiki wa timu hizi wakitarajiwa kuyapokea mabasi hayo na kuwashangilia wachezaji wakipita katika matawi.

Msafara wa timu ya Simba ukiondoka TBL Ilala utaelekea katika Tawi la Vuvuzela lililopo Makao Makuu ya klabu hiyo Kariakoo Mtaa wa Msimbazi kisha utaelekea katika Tawi la Magomeni Mpira Pesa, Ubungo katika kituo cha mabasi na hatimaye Tawi la Wailes Temeke.

Msafara wa Yanga nao ukiondoka TBL Ilala utaelekea katika Tawi la Ubungo katika kituo cha mabasi na kuelekea katika Tawi la Manzese, Lango la Jiji Magomeni, Buguruni, Mwembe Yanga, Mtoni kwa Aziz Ali, Mkombozi na hatimaye kumalizia katika makao makuu ya Jangwani, Kariakoo.

"Tunawaomba mashabiki wa timu hizi mbili wajitokeze kwa wingi katika matawi yao ili wajionee mabasi haya mapya ambayo ni ya kisasa na pia wapate fursa ya kukutana na wachezaji wa timu zao," alisema Kavishe.

Kilimanjaro Premium Lager imedhamini klabu hizi hivi tangu mwaka 2008.

0 comment.:

Post a Comment