BAO pekee la
Themi Felix katika dakika ya 67, jioni ya leo limewapa Kagera Sugar ushindi wa
1-0 dhidi ya Yanga SC, kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba katika mchezo wa Ligi
Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Felix
aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Mnigeria, Enyinna Darlington kwa
kumtungua bao hilo, kipa Mghana wa Yanga, Yaw Berko, ameendeleza rekodi yake
kuvifunga vigogo, Simba na Yanga katika Uwanja
huo.
Hiyo inakuwa
mechi ya pili Yanga kufungwa ndani ya mechi sita walizocheza hadi sasa na mbili
wametoka sare- maana yake inabaki na pointi zake nane na kuzidi kujipunguzia
matumaini ya ubingwa msimu huu, ikiwa sasa inazidiwa pointi nane na vinara wa
ligi hiyo Simba SC.
Aidha, hii
ni mechi ya pili Yanga inacheza chini ya kocha wake mpya, Mholanzi Ernie Blandts
aliyerithi mikoba ya Mbelgiji, Tom Saintfiet na katika mechi hizo mbili
ameambulia pointi moja kutokana na sare dhidi ya Simba Jumatano.
Kwa ujumla
Yanga haijashinda hata mechi moja ya ugenini kati ya tatu ilizocheza hadi sasa,
ilitoka 0-0 na Prisons, ikafungwa 3-0 na Mtibwa na leo imechapwa 1-0 na Kagera
Sugar, wakati Alhamisi itacheza na Toto African mjini
Mwanza.
Katika mechi
hiyo, Yanga ilipata pigo dakika ya 23 baada ya mshambuliaji wake mahiri na
tegemeo, Said Bahanuzi ‘Spider Man’ kuchanika nyama za paja dakika ya 23, baada
ya kugongana na beki Benjamin Effe wa Kagera Sugar na kushindwa kuendelea na
mchezo, nafasi yake ikichukuliwa na Jerry Tegete.
Tangu
ajiunge na Yanga akitokea Mtibwa Sugar msimu huu, leo Bahanuzi amecheza mechi ya
13 kwa dakika hizo 23 na ameifungia timu hiyo jumla ya mabao 12, matatu kati ya
hayo kwa penalti.
Katika mechi
hiyo iliyochezeshwa na refa Omar Juma kutoka Mwanza, aliyesaidiwa na Dominick
Nyamsana wa Dodoma na Hassan Zani wa Arusha, kikosi cha Yanga kilikuwa; Yaw
Berko, Juma Abdul, Stefano Mwasyika/nurdin, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Mbuyu
Twite, Athumani Iddi ‘Chuji’, Nizar Khalfan, Frank Domayo, Didier Kavumbangu,
Said Bahanuzi/Jerry Tegete na Haruna
Niyonzima.
Kagera;
Andrew Ntala, Jumanne Nade, Salum Kanoni, Amandus Nesta, Benjamin Effe,
Malegsesi Mwangwa, Daudi Jumanne, George Kavilla, Enyinna Darlington/Themi
Felix, Shijja Mkinna na Wilfred Emmeh/Paul Ngway.Katika mechi zilizochezwa jana, Simba SC ilizidi kujiimarisha kileleni kufuatia ushindi wa mabao 4-1 ilioupata kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam dhidi ya JKT Oljoro ya Arusha, ambayo ilimaliza pungufu ya wachezaji wawili baada ya kipa wake Shaibu Issa na mshambuliaji Meshack Nyambele kutolewa kwa kadi nyekundu kipindi cha pili.
Katika mechi
hiyo iliyochezeshwa na refa Amon Paul wa Mara, aliyesaidiwa na Anold Bugabo wa
Singida na Charles Simon wa Dodoma, hadi mapumziko Simba walikuwa tayari mbele
kwa mabao 2-1, mabao yake yote yakitiwa kimiani na kiungo Amri Ramadhan Kiemba
katika dakika za 16 na 44, wakati la Oljoro lilifungwa na Paul Nonga dakika ya
29.
Kiemba
alifunga bao la kwanza akiunganisha krosi pasi ya Christopher Edward, wakati bao
la pili lilitokana na krosi ya Nassor Masoud ‘Chollo’, yote kutokana na
mashambulizi ya upande wa kulia.
Ilikuwa
rahisi kwa Kiemba kufunga mabao yote akiwa kwenye eneo la hatari, kutokana na
mabeki wa Oljoro kumuwekea ulinzi zaidi Felix
Sunzu.
Nonga naye
alifunga bao lake baada ya kupewa pasi ndefu na kumpiga chenga kipa na Nahodha
wa Simba, Juma Kaseja upande wa kulia mwa Uwanja na kuutumbukiza mpira nyavuni
kiulaini.
Bao hilo
lilitokana na beki Paul Ngalema kupokonywa mpira wakati amepanda kusaidia
mashambulizi na Oljoro wakafanya shambulizi la
haraka.
Kipindi cha
pili Simba walirudi vizuri zaidi uwanjani na kuuteka zaidi mchezo- jambo ambalo
liliwafanya Oljoro wawapunguze kasi kwa kuwachezea rafu. Hilo liliwagharimu
kupoteza wachezaji wao wawili kabla ya filimbi ya mwisho na kufungwa mabao
mawili zaidi.
Dakika ya 83
Mganda Emanuel Okwi aliifungia Simba bao la tatu na katika dakika ya tatu ya
muda wa nyongeza baada ya kutimu dakika 90 za mchezo, Okwi akiwa anaelekea
kufunga tena, alikwatuliwa na kipa wa Oljoro Shaibu Issa na refa akaamuru
penalti sambamba na kumtoa nje kwa kadi nyekundu ya moja kwa moja mlinda mlango
huyo.
Awali ya
hapo, Oljoro ilimpoteza mchezaji mwingine, Nyambele dakika ya 78, ambaye
alionyeshwa njano ya pili kwa rafu aliyomchezea Jonas Mkude. Nahodha Kaseja
alitaka kwenda kupiga, lakini akazuiwa na Felix Mumba Sunzu akaenda kufunga bao
la nne kwa mkwaju wa penalti.
Kwa ushindi
huo, Simba imefikisha pointi 16 baada ya kucheza mechi sita, hivyo kuendelea
kuongoza Ligi Kuu, ikifuatiwa na Azam yenye pointi 13, ingawa imecheza mechi
tano.
Katika mechi
nyingine za jana, Mgambo imepata ushindi wake wa kwanza baada ya kuichapa Polisi
Morogoro 1-0, wakati Toto African imeichapa JKT Ruvu 2-1 na Prisons
imelazimishwa sare ya bila kufungana na Mtibwa Sugar.
0 comment.:
Post a Comment