UONGOZI wa
Yanga umemshauri kocha Ernie Brandts kutumia wachezaji wote badala ya kuwasahau
kabisa wengine benchi, ili uweze kubaini wachezaji ambao hawana msaada katika
timu na kuweza kuwatema katika dirisha dogo Januari,
mwakani.
Katika mechi
za karibuni, Yanga ikiwatumia wachezaji tofauti wakiwemo wale ambao wamekuwa
benchi kwa muda mrefu kama Nahodha Nsajigwa Shadrack, Nurdin Bakari na Rashid
Gumbo.
Yanga
imeweka mtego kwa wachezaji ambao wanaridhika kupewa mishahara bure bila kufanya
kazi na Januari watatupiwa virago.
Chanzo cha
habari kutoka Yanga kimesema kwamba, klabu inataka wachezaji washindani wa
namba, ili kuongeza hamasa katika timu, badala ya kuwa na wachezaji wengi wa
mazoezi tu.
Yanga
wanaonekana kucharuka sasa dhidi ya wachezaji wao kwa ujumla, kuanzia suala la
nidhamu na uwajibikaji pia, baada ya kuona wanawekeza fedha nyingi katika
usajili, lakini bado timu haichezi soka ya kuvutia, jambo ambalo wanaona
linatokana na wahezaji kubweteka.
Juzi
Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Abdallah Ahmed Bin Kleb
‘aliwawakia’ wachezaji wa mbele wa timu hiyo kwa uchoyo wa pasi na kukemea tabia
inayoonekana kuanza kujitokeza, wachezaji wa timu hiyo
kutopendana.
Bin Kleb
aliingia ‘kwa hasira’ chumba cha kubadilishia nguo cha Yanga na kuanza kufoka
juu ya tabia hiyo, akisema timu inatengeneza nafasi nyingi, lakini kwa uchoyo wa
baadhi ya wachezaji kutoa pasi kwa wenzao walio kwenye nafasi nzuri zaidi,
inaambulia mabao machache.
Bosi huyo
alifanya hivyo baada ya mechi dhidi ya Polisi Morogoro kwenye Uwanja wa Taifa,
Dar es Salaam, ambayo Yanga ilishinda 3-0.
Lakini pia
Bin Kleb alimuuliza kocha Mkuu, Mholanzi Ernie Brandts kwa nini timu haichezi
vizuri pamoja na kushinda. Brandts alitumia hekima kukwepa kujibu swali mbele ya
wachezaji, lakini baadaye alimvuta pembeni Bin Kleb
wakazungumza.
Tayari kuna
dalili za mgawanyiko ndani ya Yanga baina ya wachezaji na hilo lilijidhihirisha
wakati Hamisi Kiiza alipofunga bao lake lililokuwa la tatu katika ushindi wa
3-0, hakwenda kushangilia na wachezaji wenzake, bali alimkimbilia kipa wa akiba,
Mghana Yawe Berko kushangilia naye juzi.
Ingawa
hajawahi kulalamika, lakini ukiifuatailia Yanga tangu baada ya michuano ya Klabu
Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, Kiiza ndiye ambaye mara nyingi
amekuwa hapewi pasi na wenzake anapokuwa kwenye nafasi nzuri, ingawa yeye
amekuwa anawapa tu wenzake pasi za mabao.
Pamoja na
hayo, hali hiyo inaonekana kidogo kuathiri uchezaji wa Kiiza, anayeonekana kuwa
mnyonge na asiye na raha uwanjani na haikushangaza alipotolewa nje kipindi cha
kwanza kwenye mechi dhidi ya Simba, Oktoba 3, mwaka huu.
Lakini Kiiza
amekuwa akicheza kwa kiwango cha juu mno katika timu yake ya taifa, Uganda, The
Cranes pamoja na ‘kusuasua’ Yanga.
Yanga iko
Arusha tangu jana na imefikia katika hoteli ya Joshmal, huku ikifanya mazoezi
kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid tayari kwa mechi yao ya Ligi Kuu dhidi ya
wenyeji JKT Oljoro kesho kwenye Uwanja huo.
Yanga
inashika nafasi ya tatu katika Ligi Kuu, ikiwa na pointi 14, baada ya kucheza
mechi tisa, nyuma ya Azam FC yenye pointi 18, baada ya kucheza mechi nane,
wakati mabingwa watetezi Simba SC, wapo kileleni kwa pointi zao 19. Simba na
Azam zitacheza kesho.
0 comment.:
Post a Comment