AZAM imerejea katika nafasi ya tatu ya msimamo wa
Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwa kishindo leo baada ya kutoa kipigo kikali cha
magoli 4-1 dhidi ya Coastal Union ya Tanga katika mechi ya kwanza chini ya kocha
mpya, Stewart Hall, aliyerejea kuifundisha timu hiyo kwa mara ya
pili.
Hall, ambaye alifukuzwa
katika timu hiyo baada ya kutofautiana na uongozi kabla ya kutua katika klabu ya
Sofapaka ya Kenya aliyokuwanayo hadi aliporejea nchini jana usiku, aliendeleza
rekodi yake nzuri na Azam akiisaidia kurejea katika nafasi ya tatu baada ya
kufikisha pointi 21, mbili nyuma ya vinara Simba na Yanga wenye pointi 23 kila
moja. Azam bado ina mechi moja mkononi. Coastal imeshuka hatua moja hadi nafasi
ya nne ikiwa na pointi 19.
Kagera
Sugar ilijiimarisha katika nafasi yake ya tano kwa kufikisha pointi 17 baada ya
kuifunga Toto African 2-1 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza katika mechi
nyingine pekee ya ligi kuu iliyochezwa leo.
Kwenye Uwanja wa Azam Complex, Gaudence Mwaikimba,
ambaye amekuwa akikaa benchi kwa muda mrefu katika mechi za chini ya kocha
aliyetimuliwa Mserbia Boris Bunjak, alilipa fadhila za kuaminiwa na Hall kwa
kufunga goli la kuongoza la Azam katika dakika ya 23 akiunganisha kwa kichwa
krosi ya Khamis Mcha.
Kipre
Tchetche alifunga goli lake la sita la msimu na kuungana na Didier Kavumbagu wa
Yanga kuongoza chati ya wafungaji, baada ya kumpiga chenga kipa wa Coastal,
Jackson Chove aliyeachwa akiwa ameanguka chini katika dakika ya
36.
Mcha, aliyekuwa nyota wa
mchezo, aliifungia Azam goli la tatu baada ya kupokea pasi fupi ya Said Morad na
kupiga shuti la kustukiza lililomshinda Chove aliyeruka bila ya mafanikio na
kushuhudia timu hizo zikienda mapumziko huku wenyeji wakiwa mbele kwa magoli
3-0.
Jioni nzuri ya Mcha
ilikamilika pale alipoifungia Azam goli la nne katika dakika ya 73 kwa kupiga
shuti lililomgonga Othman Tamim wa Coastal na kutinga wavuni na wachezaji wa
Azam walithibitisha wanavyompenda kocha wao aliyerejea Hall kwa kushangilia bao
hilo kwa kumfuata mahala alipo na kumpigia makofi.
Kiungo Mkenya Jerry Santo aliifungia Coastal,
ambayo haikuonyesha upinzani uliotarajiwa, goli la kufutia machozi dakika tatu
kabla ya mechi kumalizika akitumia pasi ya fupi ya Salim Gilla.
Baada ya mechi hiyo, kocha Hall alisema
amefurahishwa na ushindi na kwamba siri ya ushindi iko mikononi mwa wachezaji
ambao wamethibitisha kwamba walikuwa wakimhitaji arejee.
Kuhusu sababu za kurejea nchini, Hall alisema njaa
ilimkimbiza Sofapaka ambako alidai kwamba wachezaji hawajalipwa kwa miezi minne
sasa na kwa kuwa Azam anaipenda moyoni mwake, alipopata tu ofa ya kurejea
alikubali mara moja.
Azam
itaikabili Yanga Jumapili katika mechi yao ijayo ya Ligi Kuu kwenye Uwanja wa
Taifa wakati vinara Simba watakuwa ugenini Morogoro dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye
Uwanja wa Jamhuri Jumamosi.
Vikosi kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi
vilikuwa;
Azam:
Ally Mwadini, Kipre Tchetche, Salim Nuhu, Ibrahim
Shikanda, Aggrey Morris, Said Mourad, Kipre Bolou/ Ibrahim Mwaipopo (dk.69),
Jabir Aziz Stima, Salum Abubakar 'Sure Boy'/ Himid Mao (dk.76), Gaudence
Mwaikimba/ Abdi Kassim 'Babi' (dk.80), Kipre Tchetche na Mcha
Khamis.
Coastal
Union:
Jackson Chove, Said Sued,
Juma Jabu, Mbwana Hamis, Jamal Machelenga/ Salim Gilla (dk.41), Jerry Santo,
Seleman Kassim 'Selembe', Razaq Khalfani/ Khamis Shango (dk.77), Daniel Lianga,
Green Atupele/ Dayton Lameck (dk.63), Othman Tamim.
4:48 PM
0 comment.:
Post a Comment