KATIKA kujiandaa na mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Kagera Sugar mjini Bukoba Jumatano, Wekundu wa Msimbazi, Simba SC leo wamecheza mchezo wa kirafiki mjini SIngida na kutoa adhabu kali ya kipigo cha mabao 4-0 kwa wenyeji, Singida United.
Katika mchezo huo uliofanyika kwenye Uwanja wa Namfua mjini Singida, mabao ya mabingwa hao wa Bara, yalitiwa kimiani na Rama Kipalamoto, Mselemu Salum, Omar Waziri ‘Inzaghi’ na Ramadhani Singano ‘Messi’.
Simba SC ambayo imewapumzisha wachezaji wake wengi wa kikosi cha kwanza na kuamua kutumia chipukizi waliopandishwa kutoka kikosi cha pili, leo ilicheza soka ya kuvutia mno.
Mashabiki wa soka mjini Singida walikuwa wakishangilia kwa nguvu burudani ya soka ya ‘Kibareclona’ na kupiga kelele timu hiyo iachane na magwiji wasio na nidhamu na kuwekeza zaidi kwa yosso hao.
Kocha Mfaransa, Patrick Liewig alitoa pendekezo la kutolewa kwa wachezaji ‘mafaza’ katika kikosi chake, kwa kuwa hawamsikilizi.
Miongoni mwa waliotengwa ni wachezaji hodari na vipenzi vya mashabiki kama Amir Maftah, Juma Nyosso, Haruna Moshi ‘Boban’ na Mwinyi Kazimoto.
Wachezaji hao makinda walicheza mechi ya kwanza ya Ligi Kuu wiki mbili zilizopita dhidi ya Coastal Union ya Tanga na kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Sasa timu hiyo inaelekeza nguvu zake katika mechi mbili za kanda ya Ziwa, ikianza na Kagera na baadaye Toto African mjini Mwanza wiki ijayo, huku wapenzi wengi wakiwa na imani na yosso wao hao.
Kwa sasa, Simba SC inashika nafasi ya tatu katika Ligi Kuu, ikiwa na pointi 34, tatu nyuma ya Azam FC inayoshika nafasi ya pili wakati Yanga SC wapo jirani kabisa na ubingwa kwa pointi zao 48 ligi ikiwa imebakiza mizunguko sita kutia nanga.
Simba SC inapambana hata kama itapoteza ubingwa, basi iipiku Azam FC katika nafasi ya pili.
Katika mchezo wa leo, kikosi cha Simba kilikuwa; Abuu Hashim, Haruna Shamte, Waziri Omar, Hassan Hassan, Hassan Khatib, Jonas Mkude, William Lucian ‘Gallas’/Said Mangela, Mselem Salum, Christopher Edward, Ramadhani Singano ‘Messi’ na Marcel Kahezya/Haroun Chanongo.
4:11 PM
0 comment.:
Post a Comment