Saturday, October 19, 2013

9:31 AM
HAPANA shaka Mrisho Khalfan Ngassa ndiye mchezaji gumzo zaidi kuelekea mchezo wa kesho wa watani wa jadi, Simba na Yanga SC akiwa amerejea Jangwani kutoka kwa mahasimu Simba SC alikocheza msimu mmoja kwa mkopo, akitoka Azam FC.
Yanga SC ilimuuza Ngassa kwa Azam Mei 21, mwaka 2010 kwa dola za Kimarekani 40,000 baada ya kuchezea timu hiyo tangu mwaka 2006.
Hata hivyo, Agosti mwaka jana aliukera uongozi wa Azam FC kwa kwenda kubusu jezi ya Yanga SC baada ya kufunga bao la ushindi katika Nusu Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame dhidi ya AS Vita ya DRC, Uwanja wa Taifa.
Baada ya kuiwezesha Azam, kutinga fainali ya michuano hiyo kwa ushindi wa 2-1, uongozi ulimuamuru kocha Stewart Hall asimpange mchezaji huyo kwenye fainali dhidi ya Yanga SC, lakini akakaidi na kumpanga na timu ikafungwa.
Kilichofuatia, Azam FC iliamua kutangaza kumuuza mchezaji huyo kwa mkopo na Simba SC wakashinda tenda hiyo, wakati Stewart alifukuzwa na kwenda Sofapaka ya Kenya.




Mserbia, Boris Bunjak aliajiriwa Azam, lakini hata kabla ya kumalizika kwa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu msimu uliopita akafukuzwa na Stewart akarejeshwa kazini.
Ngassa aligoma kuuzwa bila idhini yake, lakini Simba SC wakaketi naye mezani na kufikia makubaliano, kabla ya kumtangaza rasmi kujiunga na klabu hiyo. Baadaye Simba SC ikasema ilimuongezea Mkataba mchezaji huyo na kumpa Sh. Milioni 30, wakati yeye mwenyewe akasema alipewa fedha hizo, ili akubali kucheza kwa mkopo.
Yanga SC wakaamini maneno ya Ngassa na alipomaliza muda wake wa kuitumikia Simba SC kwa mkopo kumalizia Mkataba wake na Azam, akasaini kurejea Jangwani.
Hata hivyo, TFF ikabaini mchezaji huyo alisaini Simba SC pia hivyo kumfungia mechi sita na kumtaka arejeshe Sh. Milioni 30 na fidia ya Sh. Milioni 15. Baada ya Ngassa kulipa fedha za Simba na faini juu, akaonekana ‘kuliweka rohoni’ kwa kuwaambia Simba SC- kwamba fedha si kitu, bali utu ndiyo jambo la maana kwa wanadamu.
“Mpira ni mchezo wa furaha, hela (fedha) si kitu, kikubwa ni utu, mradi utu wangu mimi hawajauona na nimeisaidia Simba kwa kiasi kikubwa, poa, lakini pamoja na yote sina bifu nao. Ila isipokuwa michezo ni furaha, na mimi nachukulia hii kama changamoto tu,”alisema Ngassa.
Unaweza kujenga hisia kwamba Ngassa ana hasira na Simba SC na sehemu pekee ya kumalizia hasira zake ni uwanjani na nafasi ya kwanza ni kesho. Kwa sababu wengi watakwenda uwanjani pamoja na kutaka kuangalia mechi, lakini pia kuona Mrisho atafanya nini.
Kumbuka katika kipindi chote ambacho Ngassa alicheza Yanga kabla ya kwenda Azam, hajawahi kutikisa nyavu za Simba SC zaidi ya kutoa pasi za mabao tu. Na hata akiwa Simba SC hakuifunga Yanga. 

Said Mwamba Kizota (marehemu)

Kabla ya Ngassa, ni orodha ndefu ya wachezaji waliotoka Simba kwenda Yanga na kutoka Yanga kwenda Simba, tangu enzi za akina Emanuel Mbele 'Dubu', lakini ni wachache waliong'ara kote kote.
Athumani Mambosasa (sasa marehemu), Zamoyoni Mogella, Method Mogella (sasa marehemu), Hamisi Gaga (sasa marehemu), Deo Njohole, Akida Makunda, Alphonce Modest, Monja Liseki, Shaaban Ramadhan, Eustace Bajwala, Joseph Katuba (sasa marehemu) wote hao ni baadhi ya wachezaji waliotoka Simba na kwenda kucheza Yanga.
Maulid Dilunga 'Mexico', Ezekiel Greyson 'Jujuman', Justin Mtekere (wote marehemu), Ally Yussuf 'Tigana', Yussuf Macho, Godwin Aswile, Ismail Suma, Steven Nemes, Nico Bambaga, Bakari Malima, Willy Martin, Edibily Lunyamila, Mtwa Kihwelo, Omar Hussein 'Keegan', Athumani China, Mohamed Hussein 'Mmachinga', Mohamed Banka, Amri Kiemba wote pia ni baadhi ya wachezaji waliotoka Yanga na kucheza Simba. 
Athumani China akiwa Yanga, aliifunga Simba bao la mapema, dakika ya tatu, Oktoba 9, mwaka 1991 kwenye Ligi ya Muungano, wakati watoto wa Jangwani wakiibuka na ushindi wa 2-0. Bao la pili la Yanga lilifungwa na Abubakar Salum 'Sure Boy' dakika ya 54.
China tena aliifunga Yanga akiwa Simba, lilikuwa bao la pili katika ushindi wa 4-1 kwa Wekundu wa Msimbazi, Julai 2, mwaka 1994. Ally Yussuf Suleiman 'Tigana', pia alifunga mabao kote kote, Thomas Kipese kadhalika naye aliwafunga Simba na baadaye Yanga.
Akida Makunda aliihama Simba kuingia Yanga akiwa hana kumbukumbu ya kufunga bao kwenye mechi ya watani, lakini mara baada ya kutua kwa wana Jangwani aliingia kwenye orodha ya nyota waliofunga mabao kwenye mechi baina ya wababe hao wa soka ya Tanzania. 
Ilikuwa Februari 21, mwaka 1998 katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara, wakati huo ikidhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia bia yake ya Safari Lager, wakati Makunda alipofunga bao lililoelekea kuwatoa Yanga kifua mbele kwenye mchezo huo, dakika ya 46.
Lakini Athumani Macheppe alizima shangwe za wana Yanga zikiwa zimesalia dakika mbili mchezo huo kumalizika kwa bao lake safi. 
Sahau kuhusu Akida, kama yupo mchezaji ambaye aliyewapa raha mashabiki wa timu zote hizo, basi ni Said Nassor Yussuf Mwamba, maarufu kama Kizota enzi zake, aliyefariki dunia Februari 11, mwaka 2007. Kizota ni mchezaji aliyewasisimua kwa namna yake mashabiki wa Yanga na Simba kutokana na mabao yake.

Mohamed Hussein kulia na Edibily Lunyamila kushoto, walitoka Yanga SC kwenda SimbaSC

Kizota alifariki dunia baada ya kugongwa na gari eneo la Veterinary, akiwa anatoka kushuhudia mchezo wa marudiano, Kombe la Shirikisho la Soka Afrika, Raundi ya Awali kati ya wenyeji Simba dhidi ya Textil de Pungue ya Msumbiji. Alitoka kwa huzuni uwanjani siku hiyo baada ya kushuhudia timu yake ya zamani, Simba ikitolewa na wageni kwa mikwaju ya penalti 3-1, kufuatia sare ya jumla ya 2-2.
Mchezo wa kwanza Msumbiji, Simba ililazimisha sare ya 1-1 na marudiano nayo pia walibanwa kwa sare aina hiyo hiyo, hivyo kufanya mshindi aamuliwe kwa mikwaju ya penalti. Ntota ya timu ya kiwanda cha nguo Msumbiji ndiyo iliyong'ara jioni hiyo.
Kama kuna miaka ambayo Kizota alifanya vitu vya 'babu kubwa' kwenye soka ya Tanzania, basi ni 1993, kwani mapema tu mwaka huo aliibuka mfungaji bora kwenye michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati mjini Kampala, Uganda, akiiwezesha Yanga pia kutwaa ubingwa wa michuano hiyo kwa kuwafunga wenyeji, SC Villa.
Lakini pia, alikuwa mfungaji bora wa Ligi ya Tanzania. Yote tisa, kumi ni pale Kizota alipofunga mabao mawili peke yake, wakati Yanga inaibuka na ushindi wa 2-1 dhidi ya Simba kwenye mchezo wa kwanza wa Ligi ya Tanzania Bara, Uwanja wa Taifa, (sasa Uhuru) mjini Dar es Salaam. Ilikuwa ni Machi 27, mwaka huo 1993, wakati Kizota alipomchambua kipa hodari nchini enzi hizo, Mwameja Mohamed katika dakika za 47 na 57.

Zamoyoni Mogella alicheza Simba na Yanga

Simba ikielekea kulala 2-0, shukrani kwake Edward Chumila (naye marehemu pia) aliyewafungia Wekundu wa Msimbazi bao la kufutia machozi, dakika ya 75.
Baada ya kipigo kikali cha mabao 4-1, Julai 2, mwaka 1994, Yanga ilivunja kikosi ikiwafukuza karibu nyota wake wote wa kikosi cha kwanza kwa tuhuma za kuhusika kuihujumu timu katika kipigo hicho kilichotokana na mabao ya George Masatu, Athumani China, Madaraka Selemani na Dua Saidi, bao la kufutia machozi la Yanga likifungwa na beki imara, Constantine Kimanda.
Kati ya nyota waliotupiwa virago Yanga ni Kizota, ambaye kutokana na makali yake wakati huo, akiwa tegemeo la timu ya taifa ya Tanzania na miongoni mwa nyota waliotoa mchango mkubwa kwenye kikosi kilichochukua Kombe la Challenge nchini Kenya, Simba wakamwambia: "Usipate tabu Said, njoo upumzike huku".

Mrisho Ngassa akiwa na hundi za malipo ya fedha za Simba SC 

Kizota alitaka kuwaonyesha Yanga kwamba, walifanya kosa kumwacha na katika mchezo wa marudiano baina ya watani hao wa jadi wa Ligi Kuu ya Bara, Oktoba 4, 1995, Yanga ikiwa inaelekea kabisa kushinda mchezo huo 1-0, Said Mwamba alitibua furaha ya wana Jangwani dakika ya 70 kwa kufunga bao safi la kusawazisha.
Yanga ilitangulia kupata bao kupitia kwa mpachika mabao wake mahiri enzi hizo, Mohamed Hussein 'Mmachinga' dakika ya 40. Bao la Kizota liliwachanganya Yanga na dakika tisa baadaye, wakapachikwa bao la pili. Safari hiyo alikuwa ni Mchunga Bakari 'Mandela' aliyewaambia wana Jangwani; kutangulia si kufika. 
Baada ya msimu huo, Yanga walikiri kosa lao na wakaenda kumpigia magoti Kizota arejee nyumbani. Kwa sababu Kizota alikuwa anaishi nyumba ya pili kutoka klabu ya Yanga, akiishi na mkewe Tosha, Mtaa wa Jangwani, hivyo ilikuwa rahisi kumrubuni na kurejea nyumbani.
Na aliporejea Yanga, Kizota aliifunga tena Simba. Ilikuwa Novemba 9, mwaka 1996, katika sare ya ajabu ya watani, ya mabao 4-4 mjini Arusha.
Kizota aliifungia Yanga bao la kusawazisha lililofanya sare ya 3-3 katika dakika 70, baada ya awali Kipese kuifungia Simba, dakika ya saba, Edibily Lunyamila kuisawazishia Yanga kwa penalti dakika ya 28, Ahmed Mwinyimkuu kuifungia Simba la pili dakika ya 43, kabla ya Dua Said kufunga la tatu dakika ya 60 na Mustafa Hoza kuisawazishia Yanga kwa kujifunga dakika ya 64.
Sanifu Lazaro aliifungia Yanga bao lililoelekea kuwa la ushindi dakika ya 75, lakini walishindwa kulinda lango lao na kuruhusu bao la dakika za lala salama, lililofungwa na Duwa Said dakika ya 90, hivyo kuwa sare ya 4-4.   
Lakini Ngassa akiwa Yanga awali hakuifunga SImba na alipokuwa Simba hakuifunga Yanga. Sasa amerejea Jangwani na wengi wanaamini ana hasira na Simba, je atazimalizia kesho Uwanja wa Taifa? Bila shaka hilo ni jambo la kusubiri na kuona. 

0 comment.:

Post a Comment