Saturday, July 6, 2013

11:49 AM
MABINGWA wa Bara, Yanga SC wameanza mechi za kirafiki kujianda na msimu mpya kwa kutoka sare ya kufungana bao 1-1 na Express ‘Red Eagles’ ya Uganda Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza jioni hii.
Ilibaki kidogo tu, Yanga iibuke na ushindi katika mchezo huo, kama si wageni wao kupata bao la kusawazisha dakika ya 90 lililofungwa na Kivuma Winy.
Yanga SC, inayofundishwa na kocha Mholanzi, Ernie Brandts ilikuwa ya kwanza kupata bao katika mchezo huo, lililofungwa na kiungo Hamisi Thabit aliyesajiliwa kutoka African Lyon dakika ya 40.
Yanga ilijitahidi kusaka mabao zaidi, lakini washambuliaji wake Jerry Tegete na Didier Kavumbangu waliendeleza ‘ubutu’ waliomaliza nao msimu uliopita kwa kukosa mabao kadhaa ya wazi.
Katika mchezo huo, ambao Express ilionyesha upinzani kwa Yanga SC, Brandts alipanga vijana kadhaa aliowapandisha kutoka kikosi cha pili.
Kikosi kilikuwa; Deo Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Oscar Joshua, Rajab Zahir, Mbuyu Twite, Salum Telela, Nizar Khalfan/Said BahanuzI, HamisI Thabit/Bakari Masoud (Yanga B), Jerry Tegete, Didier Kavumbangu/Sospeter Mhina (Yanga B) na Abdallah Mguli (Yanga B).
Yanga kesho itarudiana na Express mjini Shinyanga kwenye Uwanja wa Kambarage na Julai 11 itacheza mechi nyingine Tabora kabla ya kurejea Dar es Salaam kuendelea na maandalizi yake ya msimu mpya.
Awali, Yanga ilitarajiwa kumenyana na mabingwa wa Uganda, KCC lakini kutokana na sababu ambazo hazikuelezwa, Wafagia Barabara wa Kampala hawakuja na imecheza na mabingwa wa zamani wa nchi hiyo, Tai Wekundu.





0 comment.:

Post a Comment