kila la kheri taifa stars.
KIKOSI cha
timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kikiwa na wachezaji 17 kimewasili
leo asubuhi jijini Gaborone tayari kwa mechi ya kirafiki ya kalenda ya
Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) dhidi ya wenyeji Botswana
'Zebras' itakayochezwa kesho.
Stars ilitua
kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Sir Seretse Khama saa 5.45 asubuhi kwa
saa za hapa ambapo nyumbani ni 6.45 na kupokewa na viongozi wa Chama cha Mpira
wa Miguu Botswana (BFA) na Watanzania wanaoishi hapa
Botswana.
Baadhi ya
wachezaji walioko kwenye kikosi hicho ni Frank Domayo, Ramadhan Singano na Simon
Msuva ambao walijiunga na Stars saa chache baada ya kurejea kutoka Nigeria
ambapo walikuwa na timu ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 (Ngorongoro
Heroes) ambayo Jumapili ilicheza mechi ya mashindano ya Afrika dhidi ya Nigeria
(Flying Eagles).
Wachezaji
wengine kwenye kikosi kilichoko Botswana ni Aggrey Morris, Amir Maftah, Athuman
Idd, Erasto Nyoni, Haruna Moshi, Juma Kaseja, Kelvin Yondani, Mrisho Ngassa,
Mwadini Ally, Mwinyi Kazimoto, Ramadhan Chombo, Salum Abubakar, Said Bahanuzi na
Shabani Nditi.
Stars
inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager imefikia kwenye hoteli ya Oasis
ambayo pia ndipo Zebras imepiga kambi kwa ajili ya mechi hiyo. Mechi itaanza
kesho saa 1 kamili usiku kwa saa za hapa na itafanyika kwenye Uwanja wa
Molepolole Sports Complex. Uwanja wa Taifa wa Botswana hivi sasa uko kwenye
matengenezo.
Kocha Mkuu
wa Taifa Stars, Kim Poulsen amesema mechi hiyo ni muhimu kwa vile timu yake bado
inakabiliwa na mechi za Kombe la Dunia Kanda ya Afrika, na michuano ya Kombe la
Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) inayotarajia kuanza baadaye mwaka
huu.
0 comment.:
Post a Comment