Taifa Stars imetoka sare ya mabao 3-3 na
wenyeji Botswana (Zebras) katika moja kati ya mechi kadhaa za kirafiki za
kalenda ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) zilizochezwa leo
(Agosti 15 mwaka huu) usiku.
Hadi mapumziko kwenye mechi hiyo iliyochezwa
Uwanja wa Molepolole ulioko Kilometa 40 nje ya Jiji la Gaborone, timu hizo
zilikuwa zimefungana mabao 2-2. Stars ndiyo iliyokuwa ya kwanza kupata bao
dakika ya 17 lililofungwa kwa penalti na beki Erasto Nyoni.
Mwamuzi Lekgotia Johannes Stars alitoa
adhabu hiyo baada ya beki Oscar Obuile Ncenga wa Zebras kumuangusha ndani ya
eneo la hatari mshambuliaji Mrisho Ngasa aliyekuwa akimkabili kipa Mompoloki
Sephekolo.
Bao hilo halikudumu muda mrefu, kwani Zebras
walisawazisha dakika ya 26 baada ya shuti kali lililopigwa na
Lemponye Tshireletso nje ya eneo la hatari
kumshinda nahodha wa Taifa Stars, Juma Kaseja. Dakika tano baadaye kiungo
mshambuliaji Mwinyi Kazimoto aliifungia Stars bao la pili kwa shuti la
mbali.
Tshireletso aliisawazishia tena Zebras
dakika ya 37. Mfungaji alifunga bao hilo kwa kichwa akiunganisha mpira wa krosi
kutoka wingi ya kushoto uliopigwa na Tebogo Sembowa ambaye kabla alimtoka beki
Aggrey Morris.
Kipindi cha pili kilianza kwa Kocha Kim
Poulsen wa Stars kuwatoa Frank Domayo na Salum Abubakar na nafasi
zao kuchukuliwa na Shabani Nditi na Athuman
Idd. Safari hii Zebras ndiyo walioanza kufunga dakika ya 69 ambapo kiungo
Michael Mogaladi aliifungia bao la tatu kwa kichwa akiunganisha krosi fupi
iliyotokana na mpira wa kurusha.
Dakika 13 za mwisho Stars walicheza pungufu
baada ya beki Erasto Nyoni kutolewa nje kwa kadi nyekundu kutokana na kumchezea
rafu mshambuliaji Lovemore Murirwa.
Mrisho Ngasa ambaye alikuwa nyota kwenye
mchezo huo aliisawazishia Stars dakika ya 84 baada ya kugongeana one-two na
mshambuliaji Simon Msuva aliyetokea benchi kuchukua nafasi ya Haruna Moshi.
"Licha ya timu kucheza vizuri, tatizo kubwa
lilikuwa kwenye safu ya ulinzi ambapo mabeki waliruhusu mipira mingi ya krosi na
kuwaacha washambuliaji wa Botswana wakifunga bila bughudha. Mabeki hawatakiwi
kuruhusu mipira ya krosi, wakiruhusu ni lazima wahakikishe wanawadhibiti
washambuliaji wa timu pinzani.
"Kwa upande wa washambuliaji, Said Bahanuzi
alikuwa akicheza mechi yake ya kwanza ya kimataifa akiwa na Stars tangu
nilipomjumuisha kwenye timu kwa mara ya kwanza. Kuna makosa madogo madogo ambayo
niliyatarajia, hivyo nitamrekebisha polepole," alisema Kocha Poulsen mara baada
ya mechi hiyo.
Stars; Juma Kaseja, Erasto Nyoni, Amir
Maftah, Aggrey Morris, Kelvin Yondani, Frank Domayo/Shabani Nditi,
Mrisho Ngasa, Salum Abubakar/Athuman Idd,
Said Bahanuzi/Simon Msuva, Haruna Moshi/Ramadhan Singano na Mwinyi
Kazimoto.
Zebras; Mompoloki Sephekolo, Tshepo
Motlhabankwe/Tshepo Maikano, Edwin Olerile, Oscar Obuile Ncenganye, Mompati
Thuma, Patrick Motsepe/Jackie Mothatego, Lemponye Tshireletso, Michael Mogaladi,
Tebogo Sembowa, Ntesang Simanyana na Galabgwe Moyana/Lovemore
Murirwa.
Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium
Lager inarejea nyumbani kesho (Agosti 16 mwaka huu) ambapo itawasili Uwanja wa
Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) saa 1.20 usiku kwa ndege ya Kenya
Airways.
0 comment.:
Post a Comment