WACHEZAJI 17 wamewekewa mapingamizi ya kusajiliwa na klabu mbalimbali za Ligi
Kuu msimu huu, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF).
Simba imewasilisha malalamiko ya mchezo usio wa
kiungwana katika usajili wa Mbuyu Twite aliyeko Yanga kwa maelezo alisaini
mkataba na klabu yao Agosti Mosi mwaka huu mbele yao, viongozi wa Shirikisho la
Mpira wa Miguu Rwanda (FERWAFA) na APR ambapo alilipwa dola 30,000 na nyingine
2,000 ikiwa ni fedha ya kujikimu na nauli yake ya kujiunga na klabu
hiyo.
Wekundu wa Msimbazi pia wanapinga Kelvin Yondani kusajiliwa Yanga
kwa maelezo kuwa ina mkataba naye uliosainiwa Desemba 23 mwaka
jana.
Yanga nayo inapinga Simba kuwaacha wachezaji Dan Mrwanda, Haruna
Shamte, Kanu Mbiyavanga na Lino Masombo kwa maelezo walishapatiwa leseni za
kucheza Ligi ya Tanzania walizozitumia kwenye mashindano ya Kombe la Kagame. Pia
inapinga Ramadhan Chombo ‘Redondo’ kujiunga Simba kwa vile ana leseni ya
kuchezea Azam kwa msimu wa 2012/2013.
Pingamizi jingine la Yanga kwa
Simba ni kuwa imezidisha idadi ya wachezaji wa kigeni wanaotakiwa kusajiliwa kwa
maelezo inao wanane wakati wanaoruhusiwa ni watano. Imewataja wachezaji hao kuwa
ni Lino Masombo, Felix Sunzu, Emmanuel Okwi, Mussa Mude, Kanu Mbiyavanga, Pascal
Ochieng, Komalmbil Keita na Daniel Akuffor.
Azam pia inapinga usajili wa
Ramadhan Chombo ‘Redondo’ kwenda Simba kwa maelezo bado ina mkataba naye
unaomalizika Juni 11 mwakani.
Toto Africans ya Mwanza imewawekea
pingamizi wachezaji Enyinna Darlinton aliyeombewa usajili Kagera Sugar, na
Mohamed Soud anayekwenda Coastal Union kwa maelezo kuwa bado ina mikataba na
wachezaji hao.
Pia Flamingo ya Arusha inapinga usajili wa wachezaji wake
Kelvin Friday Iddy katika timu za Azam na Salim Walii (Polisi Mara) kwa vile
taratibu za kuwahamisha bado hazijafanywa. Nayo Kagera Sugar inapinga usajili wa
beki David Charles Luhende kwenda Yanga kwa vile ada ya uhamisho
haijalipwa.
Super Falcon ya Chanjamjawiri, Chakechake, Pemba inapinga
wachezaji wake wanne; Edward Christopher Shija, Samir Said Luhava (Simba),
Robert Joseph Mkhotya (African Lyon) na Sultan Juma Shija (Coastal Union)
kusajiliwa katika timu hizo kwa maelezo taratibu halali za uhamisho
hazikufuatwa.
Mchezaji Othman Hassan aliyeombewa usajili Coastal Union
anapingwa na Oljoro JKT kwa vile bado ana mkataba na timu hiyo unaomalizika Mei
24, 2013. Nayo Rollingstone Multipurpose Ateclass Foundation ya Arusha inapinga
usajili wa Kigi Makassy kutoka Yanga kwenda Simba hadi itakapolipwa fidia ya
kumlea mchezaji huyo kwa vile bado hajafikisha umri wa miaka 23.
Kamati
ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya TFF chini ya Mwenyekiti wake Alex
Mgongolwa inatarajia kukutana kesho kupitia pingamizi hizo pamoja na usajili wa
wachezaji kwa ujumla kwa 2012/2013.
3:50 PM
0 comment.:
Post a Comment