Thursday, September 6, 2012

3:05 PM

KUTOKA KWA SHAFFIHDAUDI Mabingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Simba wamejikuta wakiendeshwa puta na kupata kipigo kisichotarajiwa cha mabao 3-0 kutoka kwa Sofapaka inayoshiriki Ligi Kuu ya Kenya katika mechi yao ya kimataifa ya kirafiki kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam leo.

Washindi walipata bao la utangulizi katika dakika ya 18 kwa njia ya penati baada ya beki mpya wa kimataifa wa Simba, raia wa Mali 
Komalbil Keita kucheza faulo katika eneo la boksi na mshambualiaji wa zamani wa Yanga, John Baraza akatumbukiza mpira wavuni kwa shuti lililomshinda kipa Juma Kaseja.

Safu ya mabeki wa Simba iliendelea kuwapa hofu mashabiki wa klabu yao baada ya Pascal Ochieng na keita kujichanganya na kuwapa wageni bao la pili katika dakika ya 57 kupitia tena kwa Baraza.
 

Kikosi cha Simba kinachonolewa na Mserbia Milovan Cirkovic kiliwasononesha mashabiki wao waliofika i kuwashangilia baada ya mabeki wake kuruhusu bao la tatu katika dakika ya 66 kufuatia kazi nzuri iliyofanywa na mchezaji wa zamani wa Azam, Osborne Monday kumaliziwa vyema fuatia shuti la Joseph Nyaga aliyemalizia vyema kazi nzuri iliyofanywa na mchezaji wa zamani wa klabu ya Azam, Osborne Monday.

Safu ya kiungo iliyotarajiwa kuwa 'kali' ya Salim Kinje na Mwinyi Kazimoto ilishindwa kuonyesha makali mbele ya Sofapaka, kama ilivyokuwa kwa viungo-washambuliaji Haruna Moshi 'Boban', Mrisho Ngassa aliyetua kwa kishindo katika timu hiyo akitokea Azam na mshambuliaji wao Christopher Edward aliyeibuka kinara wa kupachika mabao katika michuano iliyomalizika hivi karibuni ya Ligi ya Super8 na kuisaidia Simba B kutwaa ubingwa.

Awali, katika dakika ya 35, Simba walipata pigo baada ya Straika wao tegemeo kwa sasa, Mghana Akuffor kuumia vibaya baada ya kuchezewa faulo na Antony Kimani. 


Alianguka uwanjani na kushindwa kupumua kwa muda, lakini alipozinduka alitaka kuendelea kucheza kabla daktari wa Simba, Cosmas Kapinga kumkataza na hivyo kutolewa uwanjani. 


Kipigo cha leo kimemuacha kocha Milovan katika wakati mgumu wa kukiboresha kikosi chake kwani zimebaki siku chache kabla ya kushuka dimbani kuvaana na Azam wiki ijayo katika mechi ya kuwania Ngao ya Jamii kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
 

Kabla ya kuivaa Sofapaka leo, Milovan aliahidi soka safi na kusema kwamba mechi hiyo ndio kipimo chao kabla ya kucheza dhidi ya Azam kwani wameshajifua vya kutosha, hasa walipokuwa katika kambi yao jijini Arusha.
 

Licha ya ubutu wa safu yao ya ushambuliaji, rekodi ya mabeki wa Simba pia haionyeshi kuwa wako 'ngangari' vya kutosha tangu aondoke Kevin Yondan aliyejiunga na Yanga, kwani penati waliyoruhusu leo dhidi ya Sofapaka ni ya pili katika mechi zao nne za kirafiki za hivi karibuni. 


Penati nyingine ilishasababishwa na Pascal Ochieng. Mabeki hao vilevile wana rekodi nyingine 'mbovu' ya kujifunga mara mbili katika mechi hizo nne za kujipima nguvu, 'wadunguaji' wa mabao hayo wakiwa ni mabeki Juma Nyosso na Keita.
 



Rekodi katika mechi hizo zinaonyesha kuwa beki Ochieng aliyeondoka AFC Leopards ya Kenya kutokana na kukosa namba katika kikosi cha kwanza, alisababisha penalti moja wakati Keita ambaye ametua kutoka Mali, amejifunga goli moja na kusababisha penati moja huku Nyosso naye akijifunga moja katika mechi hizo nne ambazo Simba waliwafunga JKT Oljoro 2-1, wakawabwaga Mathare United 2-1 pia na kutoka sare ya 1-1 dhidi ya Sony Sugar ya Kenya. 



Akuffor ndiye ambaye ameonekana kuwa mchezaji 'jembe' baada ya kufunga katika mechi zote tatu za kwanza kabla ya jana kuumia.

VIKOSI
Simba: Juma Kaseja, Shomari Kapombe, Amir Maftah, Pascal Ochieng, Komalbil Keita, Mwinyi Kazimoto, Salim Kinje, Haruna Moshi ‘Boban’, Edward Christopher, Daniel Auffor na Mrisho Ngassa.

Sofapaka: Duncan Ochieng, Antony Kimani, James Situma, Edgar Ochieng, George Owino, Collins Okoti, Osborne Monday, Humphrey Mieno, Kago Danson, Joseph Nyaga na John Baraza.


Habari na picha kwa hisani ya http://straikamkali.blogspot.com/ 

0 comment.:

Post a Comment