MABAO mawili ya John Raphael Bocco ‘Adebayor’ katika dakika za 15 na 44, leo yameipa Azam FC ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Coastal Union ya Tanga katika mchezo wa kirafiki kujiandaa na mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Simba SC, Septemba 11, mwaka huu, Uwanja wa Chamazi.
Bocco alikuwa mwiba mchungu kweli leo kwa safu ya ulinzi ya Coastal, kwani pamoja kufunga mawili, lakini alikosa mabao matatu ya wazi mno. Abdulhalim Humud alitolewa nje kwa kadi nyekundu dakika ya 32 kwa rafu na lugha chafu.
Hiyo ni mechi ya tano Coastal inafungwa kati ya sita za kujipima nguvu ilizocheza kabla ya jana kufungwa 2-1 na Yanga, awali ilifungwa 3-2 na Bandari mjini Mombassa, baadaye 2-0 Tanga, ilifungwa 2-1 na Polisi mjini Morogoro na yenyewe iliifunga JKT Oljoro 1-0.
Kwa Azam hii ni mechi ya tatu mfululizo wanashinda, awali waliifunga 1-0 Prisons ya Mbeya na Transit Camp 8-0.
Azam inatarajiwa kuivaa Simba katika mechi ya Ngao ya Jamii ya kuashiria kufunguliwa kwa pazia la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Septemba 11, mwaka huu, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ikiwa ni mchezo wake wa kwanza katika historia ya Ngao hiyo.
Kihistoria hiyo itakuwa mechi ya tano ya Ngao ya Jamii kuchezwa nchini na ya pili kuishirikisha timu nje ya wapinzani wa jadi wa soka ya Tanzania, Simba na Yanga.
Mtibwa ilicheza na Yanga mwaka 2009, baada ya Simba kugoma na ikashinda mabao 2-1 na kutwaa Ngao, wakati kabla ya hapo, mwaka 2001, Ligi Kuu ya Tanzania ikiwa bado inadhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia bia ya Safari Lager, ilichezwa mechi ya kwanza ya Ngao kihistoria.
Katika mechi hiyo, Yanga ilishinda mabao 2-1 dhidi ya Simba na mwaka juzi Yanga iliifunga tena Simba kwa penali 3-1 kufuatia sare ya 0-0 na mwaka jana, Simba ilitwaa Ngao ya kwanza katika historia yake, kwa kuifunga Yanga mabao 2-0.
Ikumbukwe mara ya mwisho Simba SC ilipokutana na Azam FC, katika Robo Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame mwezi uliopita Dar es Salaam, ilifungwa mabao 3-1, yote yakifungwa na Bocco na lile la kufutia machozi kwa wekundu hao Msimbazi liliwekwa kimiani na beki mahiri Shomari Kapombe, aliyemajeruhi kwa sasa.
0 comment.:
Post a Comment