MBWANA Samatta amefunga bao
moja jioni kwenye Uwanja wa TP Mazembe mjini Lubumbashi, wakati timu yake Tout
Puissant Mazembe ikiilaza Al Ahly mabao 2-0 katika mchezo wa Kundi B, Ligi ya
Mabingwa Afrika.
Samatta alifunga bao hilo dakika
ya 49, baada ya pasi nzuri ya Tressor Mabi Mputu, kabla ya D. Kanda kufunga la
pili dakika ya 61, pasi ya Mputu tena. Thomas Ulimwengu aliingia dakika ya 67
kuchukua nafasi ya Kanda.
Mbwana ni mchezaji tegemeo wa
kikosi cha kwanza cha Mazembe kwa mwaka wa pili sasa, lakini Ulimwengu
alipandishwa kikosi hicho kwa mara ya kwanza mwezi uliopita, baada ya kukaa
kikosi cha wachezaji wa akiba tangu asajiliwe katikati ya mwaka jana na leo
amecheza mechi ya kwanza.
Mazembe imefikisha pointi10,
baada ya kucheza mechi tano, kushinda tatu, sare moja na Berekum Chelsea na
kufungwa moja na Al Ahly ugenini,
Al Ahly iliyotoa sare ya 1-1 na
Berekum Chelsea nchini Ghana katika mechi yake iliyopita, bado inaongoza kundi
hilo kwa pointi zake 10, wakati wababe wapya wa Ghana wanashika nafasi ya tatu
kwa pointi zao sita baada ya kutoka sare na Zamalek 1-1, ambao wanashika mkia
wakiwa na pointi moja.
Sasa Ahly na TPM zinawania uongozi wa kundi ili kujihakikishia kutinga Nusu Fainali kabla ya mechi za mwisho za Kundi hilo, ambazo Ahly watamaliza na Zamalek Cairo na Mazembe watamaliza Berekum Chelsea nchini Ghana
AKUFFO APIGA GOLI SIMBA
WAKITOA SARE
Akuffo |
SIMBA SC imelazimishwa sare ya
1-1 na City Stars ya Nairobi Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha jioni hii,
katika mchezo wa kirafiki kujiandaa na mechi ya Ngao ya jamii dhidi ya Azam FC,
Septemba 11, mwaka huu, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kwa matokeo hayo, Simba
imeshindwa kulipa kisasi cha Agosti 8, mwaka huu ilipochapwa mabao 3-1, Uwanja
wa Taifa, Dar es Salaam na timu hiyo.
Katika mchezo huo, bao la Simba
lilifungwa na Daniel Akuffo, wakati Komabil Keita alijifunga katika jitihada za
kuokoa na kuwapa Wakenya bao la kuongoza.
Awali, Simba ilicheza mechi
mbili Arusha, dhidi ya Mathare United ya Kenya na JKT Oljoro ya Arusha, ambazo
zote ilishinda 2-1, mshambuliaji mpya Daniel Akuffo kutoka Ghana akifunga bao
moja kila mechi, Kiggi Makaasy na Mrisho Ngassa wakifunga mabao mengine.
Simba inajiandaa na mechi ya
Ngao ya Jamii Septemba 11, mwaka huu, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ambayo
kihistoria hiyo itakuwa mechi ya tano ya Ngao ya Jamii kuchezwa nchini na ya
pili kukutanisha timu nje ya wapinzani wa jadi wa soka ya Tanzania, Simba na
Yanga.
AZAM WAICHAPA MBILI
COASTAL UNION
Bocco 'Adebayor' anasafiri |
MABAO mawili ya John Raphael
Bocco ‘Adebayor’ katika dakika za 15 na 44, leo yameipa Azam FC ushindi wa mabao
2-0 dhidi ya Coastal Union ya Tanga katika mchezo wa kirafiki kujiandaa na mechi
ya Ngao ya Jamii dhidi ya Simba SC, Septemba 11, mwaka huu, Uwanja wa
Chamazi.
Bocco alikuwa mwiba mchungu
kweli leo kwa safu ya ulinzi ya Coastal, kwani pamoja kufunga mawili, lakini
alikosa mabao matatu ya wazi mno. Abdulhalim Humud alitolewa nje kwa kadi
nyekundu dakika ya 32 kwa rafu na lugha chafu.
Hiyo ni mechi ya tano Coastal
inafungwa kati ya sita za kujipima nguvu ilizocheza kabla ya jana kufungwa 2-1
na Yanga, awali ilifungwa 3-2 na Bandari mjini Mombassa, baadaye 2-0 Tanga,
ilifungwa 2-1 na Polisi mjini Morogoro na yenyewe iliifunga JKT Oljoro
1-0.
Kwa Azam hii ni mechi ya tatu
mfululizo wanashinda, awali waliifunga 1-0 Prisons ya Mbeya na Transit Camp
8-0.
Azam inatarajiwa kuivaa Simba
katika mechi ya Ngao ya Jamii ya kuashiria kufunguliwa kwa pazia la Ligi Kuu ya
Vodacom Tanzania Bara, Septemba 11, mwaka huu, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam,
ikiwa ni mchezo wake wa kwanza katika historia ya Ngao hiyo.
Kihistoria hiyo itakuwa mechi ya
tano ya Ngao ya Jamii kuchezwa nchini na ya pili kuishirikisha timu nje ya
wapinzani wa jadi wa soka ya Tanzania, Simba na Yanga.
Mtibwa ilicheza na Yanga mwaka
2009, baada ya Simba kugoma na ikashinda mabao 2-1 na kutwaa Ngao, wakati kabla
ya hapo, mwaka 2001, Ligi Kuu ya Tanzania ikiwa bado inadhaminiwa na Kampuni ya
Bia Tanzania (TBL), kupitia bia ya Safari Lager, ilichezwa mechi ya kwanza ya
Ngao kihistoria.
Katika mechi hiyo, Yanga
ilishinda mabao 2-1 dhidi ya Simba na mwaka juzi Yanga iliifunga tena Simba kwa
penali 3-1 kufuatia sare ya 0-0 na mwaka jana, Simba ilitwaa Ngao ya kwanza
katika historia yake, kwa kuifunga Yanga mabao 2-0.
Ikumbukwe mara ya mwisho Simba
SC ilipokutana na Azam FC, katika Robo Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki
na Kati, Kombe la Kagame mwezi uliopita Dar es Salaam, ilifungwa mabao 3-1, yote
yakifungwa na Bocco na lile la kufutia machozi kwa wekundu hao Msimbazi
liliwekwa kimiani na beki mahiri Shomari Kapombe, aliyemajeruhi kwa
sasa.
0 comment.:
Post a Comment