KOCHA wa
muda wa timu ya taifa ya Kenya, Harambee Stars, James Nandwa amesikitika kumkosa
beki wa Azam FC ya Tanzania, Ibrahim Shikanda katika Kombe la Mataifa ya Afrika
Mashariki na Kati, Tusker Challenge zinazoendelea mjini
hapa.
Akizungumza
na fzakar katika mahojiano maalum mjini hapa jana, Nandwa
anayemshikia timu hiyo kwa muda Mfaransa Henri Michel, alisema kwamba alimuita
Shikanda katika kikosi chake cha Tusker Challenge, lakini akashindwa kuja kwa
sababu ni majeruhi.
“Nilimuita
Shikanda, lakini akasema yeye ni mgonjwa hawezi kuja, kwa kweli kwangu na kwa
benchi zima la ufundi tumesikitika kumkosa beki mzuri kama Yule, ambaye anafanya
vizuri hadi katika klabu yake,”alisema Nandwa.
Hata hivyo,
kocha huyo alisema kwamba anakubaliana na matokeo na ataendelea na wachezaji
alionao kuhakikisha kwamba anarejea na Kombe
Kenya.
“Michuano ni
migumu, hasa kundi letu, kama unavyoona tumefungwa na Uganda, lakini bahati
haikuwa yetu. Tulitengeneza nafasi nyingi tukashindwa kuzitumia, wenzetu
wametumia nafasi waliyopata.
Na ugumu
zaidi upo kwenye kundi. Hakuna timu dhaifu. Kuna Ethiopia ambao wamefuzu kucheza
Fainali za AFCON (Mataifa ya Afrika). Sudan Kusini umewaona wameisumbua
Ethiopia, hili ni kundi gumu sana,”alisema
Nandwa.
Hata hivyo,
amesema watapambana kushinda mechi zao zote zilizosalia ili watinge Robo
Fainali.
Kenya jana
wameanza vibaya CECAFA Tusker Challenge baada ya kuchapwa na Uganda bao 1-0
kwenye Uwanja wa Mandela, uliopo Namboole, Kampala,
Uganda.
Mbaya wao
jana alikuwa ni mshambuliaji wa Saigon Xuan Thanh ya Vietnam, Geoffrey Kizito
aliyefunga bao hilo pekee la ushindi dakika ya 74, akiunganisha krosi ya Iguma
Dennis.
Kwa ushindi
huo, Korongo wa Kampala anafungana na Ethiopia kuongoza Kundi A, kwa pointi zake
tatu kila timu.
Hadi
mapumziko hakuna timu iliyofanikiwa kuona lango la mwenzake na timu zote
zilishambuliana kwa zamu.
Kenya
walianza kwa kasi kwa dakika tano wakicheza soka iliyowasisimua mashabiki wake
wachache waliokuwapo uwanjani, lakini Uganda wakazinduka nao na kuanza kuwapa
raha mashabiki wao kwa soka safi.
Mchezo
uliendelea kuwa hivyo kwa timu hizo kushambuliana kwa zamu, kila upande
wakicheza kwa kujiamini.
Lakini sifa
ziende kwa safu zote mbili za ulinzi kutokana na kucheza kwa umakini wa hali ya
juu.
Kipindi cha
pili timu hizo ziliporejea uwanjani, zililazimika kusimama kwa takriban dakika
saba baada ya taa za uwanjani kuzimika na baada ya mafundi kutatua tatizo hilo,
ndipo kabumbu likaanza tena.
Michuno hiyo
itaendelea kesho kwa mechi mbili, Burundi na Somalia saa 10:00 jioni na baadaye
Tanzania Bara na Sudan saa 12:00 jioni.
Uganda;
Abel Dhaira/Hamza Muwonge, Iguma Dennis, Godfrey Walusimbi,Henry kalungi, Isaac
isinde, Hassan Wasswa, Geoffrey Kizito, Moses Oloya, Emmanuel Okwi, Hamisi Kiiza
na Brian Umony.
Kenya; Duncan
Ochieng, Anthony Kimani, Abdallah Juma, Jockins Atudo, David Owino, David
Ochieng, Lama Salim Mohamed, Bernard Wanyama, Humphrey Mieno, Anthony ‘Muki’
Kimani/Enock Obiero na Clifton Miheso/Paul Were.
0 comment.:
Post a Comment