SIMBA SC
imerejea Dar es Salaam leo mchana na inatarajiwa kuingia kambini moja kwa moja
kuanza maandalizi ya mechi ijayo ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, dhidi ya
Azam FC, Oktoba 27, mwaka huu, Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam.
Simba SC
itakuwa na wiki nzima ya kujiandaa na mechi hiyo, ikitoka kulazimishwa sare ya
tatu mfululizo jana kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga, baada ya kutoka 0-0
na wenyeji Mgambo Shooting katika mfululizo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania
Bara.
Matokeo
hayo, yanaifanya Simba ifikishe pointi 19, baada ya kucheza mechi tisa na
kuendelea kuongoza Ligi Kuu, ingawa wameuweka rehani usukani wa ligi hiyo kwa
Azam ambayo Jumatano inacheza na Ruvu Shooting Uwanja wa Chamazi, Dar es
Salaam.
Awali ya
hapo, Simba ilitoka 2-2 na Kagera Sugar Uwanja wa Taifa na 0-0 na Coastal Union
Uwanja wa Mkwakwani.
Azam yenye
pointi 17, ikishinda itafikisha pointi 20 na kupanda kileleni, tena ikiwa nyuma
kwa mchezo mmoja, kwani hadi sasa imecheza mechi saba. Yanga iliyocheza mechi
nane, ina pointi 14 katika nafasi ya tatu nayo itacheza na Polisi Morogoro
keshokutwa.
Katika mechi
ya jana ya Simba na Mgambo, iliyochezeshwa na refa Athumani Lazi wa Morogoro,
dakika 45 za kwanza, timu zote zilishambuliana kwa zamu na zilionyesha kiwango
kizuri, ushindani mkubwa- kwa ujumla ilikuwa burudani.
Kipindi cha
pili kadhalika pamoja na kocha Mserbia, Profesa Milovan Cirkovick kufanya
mabadiliko akiwatoa Mrisho Ngassa na Amri Kiemba na kuwaingiza Edward
Christopher na Salim Kinje, bado walishindwa kuifunga Mgambo iliyopanda Ligi Kuu
msimu.
Katika
dakika 10 za mwisho, ilishuhudiwa Mgambo wakicheza kwa kujihami zaidi kutokana
na presha kali ya mashambulizi ya Simba SC.
Katika mechi
hiyo, kikosi cha Mgambo kilikuwa; Godson Mmasa, Yassin Awadh, Salum Mlima,
Bakari Mtama, Salum Kipanga, Ramadhani Malima, Chande Magoja/Nassor Gumbo dk85,
Mussa Ngunda, Issa Kandulu, Fully Mganga na Juma
Mwinyimvua.
Simba
SC;Juma Kaseja, Nassor Masoud ‘Chollo’, Amir Maftah, Hassan Hatibu, Paschal
Ochieng, Jonas Mkude, Amri Kiemba/Salim Kinje dk88, Mwinyi Kazimoto, Felix
Sunzu, Emmanuel Okwi na Mrisho Ngassa/Edward Christopher dk 79
0 comment.:
Post a Comment