TIMU ya soka
ya Mgambo JKT ya mjini Handeni mkoani Tanga, imeondoka leo mjini Tanga,
ilikokuwa imeweka kambi kwenda Dar es salaam ambako kesho itashuka dimbani
kwenye Uwanja wa Taifa kucheza na wenyeji Yanga katika mfululizo wa Ligi Kuu ya
Vodacom Tanzania Bara.
Mgambo
inayoshika nafasi ya 10 kwenye msimamo wa Ligi Kuu hadi sasa kwa kuwa na pointi
10 ikiwa imecheza michezo tisa, imeondoka na wachezaji wake 22 na viongozi
watatu kwa ajili ya pambano hilo ambalo timu hiyo ilisema kuwa inalichukulia kwa
umakini mkubwa ili waweze kuibuka na ushindi kutokana na kujiandaa
vilivyo.
Kocha Mkuu
wa timu hiyo Mohamed Kampira, alisema jana mjini hapa kwamba, Yanga
waailichukulie kuwa watawafunga kirahisi katika mchezo huo badala yake wategemee
kupata upinzani hasa kutokana na kwamba timu hiyo ya Mgambo imejiandaa kuibuka
na ushindi ili waweze kukaa katika nafasi nzuri katika mzunguko huu wa
kwanza.
"Tunaondoka
kesho asubuhi (leo) kwenda Dar es salaam, kama timu tumejiandaa vizuri na
tunatarajia kuwapa wakati mgumu Yanga na kuishinda, wasitarajie mteremko, sisi
ni timu na tunaamini kwamba tutaibuka na pointi zote tatu," alisema kwa
kujiamini Kampira aliyevaa viatu vya aliyekuwa kocha mkuu wa timu hiyo Stephen
Matata aliyetimuliwa baada ya timu hiyo kuanza vibaya kwa kufungwa michezo
mitano mfululizo tangu kuanza kwa ligi hiyo.
Kampira
alisema hadi sasa wachezaji wake wamekuwa na ari kubwa ya kuibuka na ushindi na
hakuna majeruhi wote wapo katika hali nzuri ya kupambana na timu hiyo inayousaka
ubingwa mwaka huu kwa udi na uvumba na kwamba amewata mashabiki wa timu hiyo
kuiamini kwa wachezaji watafanya kazi
iliyokusudiwa.
Mgambo JKT
ambayo baada ya kumtimua kocha ilikuwa imeshikwa na kocha msaidizi Josepj Lazaro
ambaye aliipa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Polisi Morogoro, akaifunga Mtibwa
Sugar bao 2-1 kwenye uwanja wa Manungu, ikaifunga Toto African bao 2-0 na
ikatoka sare ya 0-0 na Simba mchezo ambao Kampira ilikuwa ni mchezo wake wa
kwanza kukaa kwenye benchi la timu hiyo.
Wakati huo
huo, mashabiki wa klabu ya Coastal Union ya Jijini hapa, wameipongeza timu yao
kwa ushindi walioupata juzi walipoifunga JKT Ruvu bao 3-0 katika mchezo
uliofanyika kwenye uwanja wa Azam Complex, Chamazi Jijini Dar es salaam hatau
ambayo walisema inatia faraja na wamewataka wacheji wazidi kuongeza bidii ili
lengo la kumaliza ikiwa nafasi za juu litimie.
Mmoja wa
mashabiki hao Fred Tayasar alisema wamejisikia furaha ushindi huo lakini pia
umewapa majonzi makubwa kwa mchezaji wao Nsa Job kuvunjika mguu katika pambano
hilo hatua ambayo alisema wapenzi wa timu hiyo wanaangalia uwezekano wa
kumchangia fedha kwa ajili ya kumpa ili aweze kujikimu katika kipindi
atakachokuwa nje ya uwanja.
0 comment.:
Post a Comment