Mabao kutoka kwa straika wa kimataifa wa Burundi,
Didier Kavumbagu na straika wa Uganda, Hamis Kiiza yaliipandisha Yanga kileleni
mwa msimamo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya kuibuka na ushindi 'mtamu' wa
mabao 2-0 dhidi ya Azam kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam huku
mahasimu wao wa jadi, Simba wakipata kipigo cha ugenini cha 2-0 kutoka kwa
Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro leo.
Kama ilivyokuwa
kwa Yanga, Mtibwa walifunga mabao yao pia katika kila kipindi kupitia kwa
mastraika wao nyota, Said Mkopi na Hussein Javu ambaye aliwahi pia kuiliza Yanga
kwa kupiga 'hat-trick' wakati 'Wanajangwani' walipolala3-0 katika mechi yao ya
raundi za mwanzo wa msimu.
Katika mechi ya Taifa, Yanga walionyesha soka
safi kuanzia mwanzo wa mechi hadi mwisho, wakigongeana pasi za kuvutia na
kutawala mno katika eneo la katikati ya dimba lililokuwa chini ya himaya ya
kiungo wao wa kimataifa kutoka Rwanda, Haruna Niyonzima
'Fabregas'.
Kavumbagu aliifungia Yanga bao la utangulizi katika kipindi
cha kwanza na Kiiza alifunga goli la pili lkatika kipindi cha pili ambacho Azam
walijikuta wakiusaka mpira kwa tochi kutokana na 'gonga' za kusisimua za Yanga;
zikiwamo zilizozaa bao la Kiiza baada ya Fabregas, Kiiza na Chuji kupigiana
'one-two' kabla mfungaji kukwamisha mpira wavuni.
Matokeo ya mechi za leo
yameifanya Yanga ikwee rasmi kileleni mwa msimamo wa ligi kuu ya Bara kwa mara
ya kwanza msimu huu, ikifikisha pointi 26 na kuwaacha mahasimu wao wa jadi,
Simba wanaoshika nafasi ya pili kwa tofauti ya pointi tatu. Azam inaendelea
kubaki katika katika nafasi yake ya tatu ikiwa na pointi 21.
Kipigo cha
leo kwa Simba inayoonekana kama ilitangulia na "baiskeli ya barafu" ni
muendelezo wa matokeo mabaya kwa 'wekundu' hao, hasa katika mechi zao za ugenini
kwani licha ya kuongoza kwa muda mrefu kutokana na ushindi mfululizo wa mechi
zao nyingi za nyumbani; mabingwa hao watetezi walijikuta wakishikiliwa kwa sare
dhidi ya Coastal Union na Mgambo JKT za Tanga, Kagera Sugar waliyocheza nayo
kwenye Uwanja wa Taifa na pia wakasimamishwa kwa sare ya ugenini pia kwenye
Uwanja wa Jamhuri, Morogoro dhidi ya 'maafande' wa Polisi Moro ambao ndiyo
wanaoburuta mkia kwenye msimamo wa ligi hiyo.
8:10 AM
0 comment.:
Post a Comment