KAMA ingekuwa ni ndondi, leo Tanzania wangetawazwa kuwa mabingwa wapya wa Afrika, baada ya kuwapiga Zambia, lakini katika soka, haiku hivyo.
Tanzania, Taifa Stars leo imeendeleza wimbi lake la ushindi katika michezo ya kirafiki baada ya kuifunga Zambia 1-0, kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Katika mchezo wa leo, hadi mapumziko, tayari Stars ambayo Novemba 14, mwaka huu iliifunga 1-0 Kenya, Uwanja wa CCM Kirumba, walikuwa mbele kwa bao 1-0 lililowekwa kimiani na kiungo mshambuliaji Mrisho Khalfan Ngassa.
Ngassa, anayecheza kwa mkopo Simba SC akitokea Azam FC, zote za Dar es Salaam, alifunga bao hilo dakika ya 45, akimalizia pasi nzuri ya kiungo wa Simba SC, Mwinyi Kazimoto.
Stars ilicheza vizuri na kwa umakini wa hali ya juu kipindi cha kwanza, na kufanikiwa kuwabana mabingwa hao wa Afrika wanaojiandaa kwenda kutetea taji lao nchini Afrika Kusini mapema mwakani.
Kipindi cha pili, Zambia walianza kwa kurekebisha kikosi chao, kocha Mfaransa, Herve Renard akiwatoa Hichani Himonde, Moses Phiri, Sinkala na Isaac Chansa na nafasi zao kuchukuliwa na Stopila Sunzu, Mukuka Mulenga, Evans Kangwa na Francis Kasonde.
Pamoja na mabadiliko hayo, Stars iliendelea kung’ara na katika dakika ya 57 Ngassa alikaribia kufunga tena kama si shuti lake kufuatia pasi ‘tamu sana’ ya Sure Boy kutoka nje.
Lakini kukosa kwa Ngassa bao hilo, kulitokana na maarifa ya beki wa TP Mazembe ya DRC, Stopila Sunzu anayejiandaa kuhamia Reading ya England, ambaye alimbana kiungo huyo wa Simba kumynima mwanya wa kupiga vizuri na akafanikiwa kumfanya apige nje.
Zambia walipoteza nafasi nzuri ya kusawazisha bao dakika ya 76, baada ya shuti la Chasamba Lungu kugonga mwamba, wakati kipa Juma Kaseja akiwa amekwishapotea maboya.
Ngassa alijibu shambulizi hilo dakika ya 77 baada ya shuti alilojaribu kupaa juu ya lango, huku Felix Katongo akipewa kadi ya njano, baada ya kumuangusha Amri Kiemba aliyekuwa anamfunga tela.
Juma Kaseja alifanya kazi ya ziada dakika ya 86, baada ya kuokoa shuti la karibu la Chris Katongo na katika dakika ya 87, Stars ilipata pigo baada ya beki Kevin Yondan kuumia na nafasi yake kuchukuliwa beki mwenzake wa Yanga, Nadir Haroub Ally ‘Cannavaro’ dakika ya 88.
Kikosi cha Stars leo kilikuwa; Juma Kaseja, Erasto Nyoni, Shomari Kapombe, Aggrey Morris, Kevin Yondan/Nadir Haroub dk 87, Frank Domayo, Salum Abubakar, Mwinyi Kazimoto, Amri Kiemba, Mrisho Ngassa/Amir Maftah dk83 na Khamis Mcha ‘Vialli’/Simon Msuva dk59.
Zambia; Danny Munyao, Chintu Kampamba, Hichani Himonde, Chisamba Lungu, James Chamanga, Moses Phiri, Chris Katongo, Felix Katongom Nathan Sinkala/, Rodrick Kabwe na Isaac Chansa.
0 comment.:
Post a Comment