Kocha mpya wa Simba, Mfaransa Patrick Liewig
ametua nchini leo na kupokewa na mamia ya mashabiki wa 'Wanamsimbazi' huku
akiahidi kuwaletea mafanikio makubwa mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu ya
Tanzania Bara.
Akizungumza na
waandishi wa habari baada ya kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius
Nyerere jijini Dar es Salaam, Liewig aliyekuja kutwaa nafasi iliyoachwa wazi na
Mserbia Milovan Cirkovic, amesema 'Wanamsimbazi' watarajie mambo mazuri kutoka
kwake, lakini kwa sharti la kumpa ushirikiano katika kila hatua wakati
atakaposaini mkataba wa kuifundisha timu hiyo na kuanza kibarua
chake.
"Nimefurahishwa sana na mapokezi haya... najihisi kuwa
nina deni kubwa. Naamini nitapata ushirikiano wa kutosha na baada ya kuzoeana na
wachezaji, naamini Simba itafika mbali katika kila michuano," alisema kocha
huyo.
Miongoni mwa watu waliofika uwanjani kumpokea kocha
huyo ni Katibu Mkuu wa Simba, Evodius Mtawala, ambaye aliwaongoza mamia ya
mashabiki wa Simba kumpokea kwa maandamano ya magari na pikipiki za bodaboda na
bajaji.
Taarifa kutoka ndani ya Simba zinaeleza kuwa kocha huyo
atasaini mkataba wa kuifundisha klabu hiyo kwa miezi 18 na tukio hilo
litakamilishwa kesho.
12:49 PM
0 comment.:
Post a Comment