MSHAMBULIAJI Mohamed Hussein, jioni ya leo ameinusuru Toto Africans kuzama mbele ya Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Manungu, Turiani, Morogoro baada ya kuifungia mabao mawili dakika za lala salama na kufanya sare ya 2-2 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Hadi mapumziko, tayari Mtibwa Sugar walikuwa mbele kwa mabao mawili yaliyowekwa kimiani na Juma Luzio dakika ya pili na Hassan Salum dakika ya 14.
Wakati dakika zikiyoyoma na Mtibwa wakiwa tayari wana matumaini ya kubeba pointi tatu, Mohamed Hussein alicharuka ghafla na kufunga katika dakika za 73 na 88.
Sare hiyo, inaifanya Mtibwa ifikishe pointi 33 baada ya kucheza mechi 23 na kuendelea kukaa nafasi ya tano nyuma ya Simba SC yenye 35, wakati Toto inafikisha pointi 23 baada ya kucheza mechi 24 na inabaki nafasi ya 11.
Katika mechi nyingine za ligi hiyo leo, Tanzania Prisons wameutumia vyema Uwanja wa nyumbani, Sokoine mjini Mbeya kwa kuwalaza 1-0 JKT Mgambo, bao pekee la Nurdin Issa dakika ya 14, wakati Polisi Morogoro imetoka sare ya bila kufungana na Ruvu Shooting Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.
Ruvu inabaki nafasi ya saba kwa pointi zake 30 baada ya kucheza mechi 21, Mgambo inabaki nafasi ya tisa kwa pointi zake 24 baada ya kucheza mechi 22, Prisons inapanda kwa nafasi mbili hadi ya 10 kwa kufikisha pointi 23 baada ya kucheza mechi 23 na Polisi Moro inapanda kwa nafasi moja hadi ya 13 baada ya kufikisha pointi 19, sawa na African Lyon inayoshika mkia zikizidiana wastani wa mabao ya kufunga na kufungwa tu.
5:55 PM
0 comment.:
Post a Comment