RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amewaahidi ‘neema’ wachezaji wa timu ya soka ya taifa, Taifa Stars iwapo watafanikiwa kushinda mechi zote tatu za mzunguko wa pili katika Kundi D, kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe a Dunia mwakani nchini Brazil.
Akizungumza nao Ikulu mjini Dar es Salaam leo, Rais Kikwete alisema kwamba amefarijika sana na matokeo ya sasa ya timu hiyo, chini ya Kocha Mdenmark, Kim Poulsen na akawataka kuongeza juhudi kuhakikisha wanamaliza wakiwa wanaongoza Kundi C.
Amesema iwapo watafanya hivyo, atawafanyia kitu kizuri ambacho kitakuwa kumbukumbu nzuri katika maisha yao ya soka hata wakistaafu.
Rais Kikwete amesema kwamba huwa anaumia sana timu hiyo inapofanya vibaya, kiasi cha kukosa hata raha mbele ya viongozi wenzake wa nchi nyingine wanaofuatilia soka anapokutana nao na kumuuliza matokeo ya Taifa Stars.
“Wakati fulani mlifungwa na Msumbiji mechi ilichezwa usiku, mimi nilikuwa Arusha kwenye mkutano na Marais wenzangu, asubuhi yake wakaniuliza vipi matokeo ya mechi ya jana, kwa kweli nilikosa raha, niliwajibu hatukucheza vizuri sana na tulifungwa,”alisema.
Rais Kikwete alisema anajua mchezo unaofuata dhidi ya Morocco Juni 8, mwaka huu mjini Marakech utakuwa mgumu kwa Stars, kwa sababu mechi iliyopita Tanzania iliifunga timu hiyo mabao 3-0 Dar es Salaam.
“Lazima watakuwa wagumu kufungwa tena, najua utakuwa mchezo mgumu, lakini kajitahidini muwafunge tena, ili mradi kwanza mmalize mnaongoza hili Kundi, halafu mtaona tumewaandalia nini,”alisema.
Rais pia alimpongeza Kocha Poulsen kwa kuifikisha Stars sehemu nzuri na akamtaka kuongeza bidii kuhakikisha anaendeleza wimbi la ushindi, kwani timu ikianza kufanya vibaya hali itakuwa mbaya.
Rais pia aliipongeza Kamati ya Saidia Stars Ishinde, ambayo juzi iliwapa Sh. Milioni 30 wachezaji wa timu hiyo kama hamasa ili wafanye vizuri.
Rais aliisifu Kamati hiyo kwamba inaundwa na watu ambao wanaijua soka, hivyo shaka itafanya kazi yake vizuri.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Saidia Stars Ishinde, Dk Ramadhani Dau alisema watahakikisha wanafanya jitihada Stars ifanye vizuri.
Dk Fenella Mukangara |
Dk Ramadhani Dau |
Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Dk Fenella Mukangara naye aliwapongeza wachezaji wa Stars na kocha wao na akawataka kuongeza bidii ili kupata matokeo mazuri zaidi.
Nahodha wa Stars, Juma Kaseja alimshukuru Mheshimiwa Rais na kusema kwamba watakwenda kupigana kwa uwezo wao wote kuhakikisha wanapata matokeo mazuri.
Rais Kikwete aliwaalika wachezaji wa Stars chakula cha mchana Ikulu mjini Dar es Salaam na baada ya chakula hicho ndipo akatoa hutuba hiyo.
Kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’ wa Azam FC, hakuwepo Ikulu leo kutokana na kufiwa na baba yake mlezi usiku wa jana, wakati Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wataungana na timu Marakech kutoka DRC, wanakochezea TP Mazembe.
Wachezaji waliokuwapo Ikulu leo ni makipa; Nahodha Juma Kaseja (Simba), Aishi Manula (Azam), Ally Mustafa (Yanga) na Mwadini Ally (Azam). Mabeki ni Aggrey Morris (Azam), Erasto Nyoni (Azam), Kelvin Yondani (Yanga), Nadir Haroub (Yanga), Shomari Kapombe (Simba), Vincent Barnabas (Mtibwa Sugar) na Waziri Salum (Azam).
Viungo ni Amri Kiemba (Simba), Athuman Idd (Yanga), Frank Domayo (Yanga), Haruna Chanongo (Simba), Khamis Mcha (Azam), Mwinyi Kazimoto (Simba) na Mudathiri Yahya (Azam).
Washambuliaji ni John Bocco (Azam), Juma Luzio (Mtibwa Sugar), Mrisho Ngasa (Simba), Simon Msuva (Yanga) na Zahoro Pazi (JKT Ruvu).
Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager, imeweka kambi katika hoteli ya Tansoma, Dar es Salaam ikiendelea kujinoa kwa ajili ya mechi hiyo ambayo itatanguliwa na mchezo wa kujipima nguvu dhidi ya Sudan, Nile Crocodiles Juni 2 mwaka huu mjini Addis Ababa, Ethiopia.
Hadi sasa, Stars inashika nafasi ya pili katika Kundi C, ikiwa na pointi sita baada ya kucheza tatu kushinda mbili na kufungwa moja, nyuma ya Ivory Coast yenye pointi saba, iliyoshinda mechi mbili na kutoa sare moja.
Kama Stars itashinda ugenini dhidi ya Morocco, itajiweka katika nafasi nzuri ya kuingia kwenye hatua ya mwisho ya kuwania tiketi ya Brazil, kwani ikiongoza Kundi hilo, itacheza mechi mbili za mwisho nyumbani na ugenini dhidi ya moja ya timu zilizoongoza makundi ambayo ikishinda itaweka historia ya kucheza Fainali za Kwanza za Kombe la Dunia.
Stars, imekuwa na mwenendo mzuri chini ya Mdenmark Kim Pouslen, ambaye ameiwezesha kushinda mechi tano kati ya 10, sare tatu na kufungwa mbili tangu aanze kazi Mei mwaka jana, akirithi mikoba ya Mdenmark mwenzake, Jan Poulsen.
Awali TFF ilikuwa imeitafutia Taifa Stars mechi ya kirafiki Juni 1, mwaka huu dhidi ya Algeria, Libya au Misri. Lakini baadaye Algeria ikasema itacheza na Togo, wakati Misri ilitaka mechi hiyo ichezwe Juni 4 jijini Cairo, jambo ambalo lisingewezekana kwa Stars kwani ina mechi ya mashindano Juni 8 mwaka huu.
Kwa upande wa Libya mechi hiyo ilikubaliwa ichezwe Tunis, Tunisia, Juni 2 mwaka huu. Lakini baadaye Libya ikataka mechi hiyo ichezewe jijini Tripoli ambapo TFF ilikataa kutokana na sababu za kiusalama.
0 comment.:
Post a Comment