Sunday, August 4, 2013

1:50 PM
BAADA ya jana Simba SC kulazimishwa sare ya kufungana 1-1 na kombaini ya Polisi, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, wapinzani wao wa jadi, Yanga SC leo wameibuka na shangwe kwenye Uwanja huo kwa ushindi wa mabao 3-1 katika mfululizo wa mechi za kujiandaa na msimu.

Katika mchezo wa leo, hadi mapumziko, tayari Yanga SC walikuwa mbele kwa bao 1-0, lililotiwa kimiani na Said Bahanuzi ‘Spider Man’ dakika ya 26, baada ya kutokea piga nikupige langoni mwa Wakata Miwa wa Manungu.Katika kipindi hicho cha kwanza, Mtibwa Sugar walipata nafasi kadhaa za kufunga wakashindwa kuzitumia. Mtibwa walikuwa wa kwanza kubisha hodi langoni mwa Yanga SC dakika ya tano na Shaaban Kisiga ‘Malone’ alipiga shuti lililotoka nje.Yanga wakajibu shambulizi dakika ya tisa, lakini Shaaban Kondo alishindwa kuunganisha pasi nzuri ya Bahanuzi, ambaye leo amedhihirisha ameanza kurejea katika kiwango chake kile kiliochompa ufungaji bora wa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame mwaka jana.  Bahanuzi alikaribia kufunga kwa mpira wa adhabu dakika ya 15, kufuatia Jerry Tegete kuangushwa nje kidogo ya eneo la hatari, lakini shuti lake likaenda nje sentimita chache kabla ya kufanya kweli dakika ya 26.Mtibwa walifanya jaribio la kusawazisha dakika ya 35, lakini Salum Mbonde akapiga nje akiwa kwenye nafasi nzuri na dakika ya 41, Tegete naye alikaribia kufunga kama si shuti lake kutoka nje.Mtibwa tena walikaribia kusawazisha dakika ya 45 kama si shuti la Kisiga kutoka nje.  Kipindi cha Yanga walianza kwa mabadiliko ambayo yaliongeza uhai kwenye timu yake, hususan Hussein Javu aliyesajiliwa majira haya ya joto kutoka Mtibwa, aliyeingia kuchukua nafasi ya Shaaban Kondo. Javu alifumua shuti zuri dakika ya 51, kipa Hussein Sharif ‘Cassilas’ akadaka.Hatimaye jitihada za Kisiga zilizaa matunda dakika ya 57 baada ya kuisawazishia bao timu yake kwa penalti, kufuatia beki aliyesajiliwa Yanga SC kutoka Mtibwa, Rajab Zahir kuunawa mpira katika eneo la hatari na kipa Ally Mustafa ‘Barthez’ aliyempokea Deo Munishi ‘Dida’ hakuweza kuinusuru timu yake na pigo hilo.  Jerry Tegete aliifungia Yanga SC bao la pili kwa penalti dakika ya 81, baada ya yeye mwenyewe kuangushwa kwenye eneo la hatari na beki wa Mtibwa, Salvatory Ntebe wakati anaelekea kufunga.Hussein Javu aliisulubu timu yake ya zamani, Mtibwa dakika ya 87 baada ya kutumia vyema makosa ya kipa aliyetemwa Yanga na kuangukia kwa Wakata Miwa hao, Said Mohamed kuwafungia wana Jangwani bao la tatu. Kikosi cha Yanga SC leo kilikuwa; Deo Munishi ‘Dida’/Ally Mustafa ‘Barthez’ dk46, Juma Abdul, Oscar Joshua/David Luhende dk46, Issa Ngao, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Athumani Iddi ‘Chuji’/Rajab Zahir dk46, Said Bahanuzi/Abdallah Mnguli ‘Messi’ dk 71, Salum Telela, Shaaban Kondo/Hussein Javu dk46, Jerry Tegete na Haruna Niyonzima.Mtibwa Sugar; Hussein Sharif ‘Cassilas’/Said Mohamed dk53, Hassan Ramadhani, Paul Ngalema, Ally Lundenga/Dickson Daudi dk64, Salvatory Ntebe, Salum Mbonde, Ally Shomari, Masoud Ally, Abadallah Juma, Shaaban Kisiga ‘Malone’ na Ally Mohamed ‘Gaucho’.

0 comment.:

Post a Comment