MENEJA Mkuu
wa klabu ya African Lyon ya Dar es Salaam, inayoshiriki Ligi Kuu ya Vodacom
Tanzania Bara, Rahim Kangezi ‘Zamunda’ kesho anatarajiwa kuchukua fomu za
kuwania nafasi ya Ukatibu Mkuu wa Chama cha Soka Dar es Salaam
(DRFA).
Zamunda kama
atachukua fomu hiyo kesho, ina maana mpinzani wake mkuu atakuwa Katibu wa sasa
wa DRFA, Msanifu Kondo, ambaye amejijengea ngome imara katika kampeni kwa muda
mrefu.
Akizungumza
na Fzakar.blogspot.com mida hii, Zamunda amesema kwamba awali nia yake
ilikuwa kuchukua fomu ya kugombea Uenyekiti, lakini ameona tayari
wamekwishajitokeza watu wenye sifa, hivyo anahamia kwenye
Ukatibu.
“Mimi ni
mtendaji mzuri hakuna shaka katika hilo, watu wameona nilipoitoa African Lyon
hadi nilipoifikisha, nimewasaidia wachezaji wengi wa Tanzania kwenda Amerika na
Ulaya kucheza soka ya kulipwa,”.
“Nimekuwa
mwanaharakati wa haki za klabu za Ligi Kuu na kwa kiasi kikubwa hadi kufikia
hapa klabu zinaelekea kujikomboa, kuna mchango wangu mkubwa. Sasa nataka niingie
DRFA kufanya mapinduzi makubwa ya kimaendelea ya mpira na
uchumi.”.
“Nataka DRFA
isiwe tu ya kutegemea migawo ya mapato ya milangoni kutoka TFF, bali iwe na
uwezo wake wa kujitegemea na kujiendesha. Iwe na wafadhili wa maana na
wadhamini, tena kwa mikataba ya maandishi,”alisema Zamunda na
kuongeza.
“Nataka
nifanye mapinduzi makubwa katika soka Dar es Salaam, kampuni kubwa itakuwa
mdhamini wa DRFA, klabu na wadau wa soka Dar es Salaam watanufaika sana,
wachezaji wa Dar es Salaam watanufaika
sana,”alisema.
Zamunda
ndiye aliyempatia Nizar Khalfan nafasi ya kucheza Ligi Kuu ya Marekani, ambako
alichezea klabu ya Vancouver Whitecaps na baadaye Philadelphia Union kabla ya
kurejea nyumbani.
Akiwa huko,
Nizar alipata fursa ya kuichezea Vancouver dhidi ya timu kadhaa za Ligi Kuu ya
England, ikiwemo dhidi ya Manchester City mwaka juzi katika michezo ya
kirafiki.
Zamunda pia
alimpatia Mrisho Ngassa nafasi ya kwenda kufanya majaribio Seattle Sounders ya
Marekani ambako alipewa nafasi ya kucheza mechi dhidi ya Manchester United mwaka
juzi pia.
Mchakato wa
uchaguzi wa DRFA unazidi kupamba moto na katika nafasi ya Uenyekiti, Ahmad Seif
Hemed anachuana na Salum Mkemi, Evans Aveva, Ayoub Nyenzi, Juma Jabir na Meba
Ramadhan, ambao ndio pekee hadi sasa wamechukua
fomu.
Wagombea
wengine waliochukua fomu hadi jana ni Ally Mayay, nafasi ya Makamu Mwenyekiti,
Said Tuliy, Hamisi Ambari, ambao wanawania nafasi ya Ukatibu Mkuu, Shaffi Dauda
na Muhisn Balhabou, Ujumbe wa Mkutano Mkuu, Shaaban Mohamed, Andrew Tupa, Siza
Abdallah Chenje, Sunday Mwanahewa na Lameck Nyambaya Ujumbe wa kamati ya
Utendaji na Philemon Ntahilaja, Mwakilishi wa Klabu.
Uchaguzi wa
DRFA utafanyika Desemba 8, mwaka huu na fomu za kugombea nafasi mbalimbali
zilianza kutolewa tangu Oktoba 29, wakati Novemba 4 hadi 8, Kamati ya Uchaguzi,
chini ya Mwenyekiti wake, Juma Simba itapitia fomu za walioomba
uongozi.
Novemba 9
hadi 13 utakuwa muda wa pingamizi kwa wagombea, ambazo zitajadiliwa Novemba 14
hadi 16, wakati Novemba 17 hadi 19 watatoa fursa ya kukata rufaa, ambazo
zitasikilziwa Novemba 20 hadi 24 na baada ya hapo, Novemba 25 yatatangazwa
majina ya wagombea waliopitishwa.
Uchaguzi wa
DRFA utafanyika siku chache tu kabla ya uchaguzi wa Shirikisho la Soka Tanzania
(TFF), mwishoni mwa Desemba, mwaka huu.
0 comment.:
Post a Comment